Oct 04, 2022 02:22 UTC
  • Somalia: Tumemuangamiza mwasisi wa genge la al Shabaab katika operesheni maalumu

Serikali ya Somalia imesema kuwa imemuangamiza mmoja wa waanzilishi wa genge la kigaidi la al Shabaab katika operesheni ya pamoja iliyofanywa na nchi hiyo kwa kushirikiana na waitifaki wake wa kimataifa mwishoni mwa juma.

Tangazo hilo la serikali ya Somalia limetolewa baada ya magaidi wa al Shabaab kudai kuhusika na shambulio jipya la jana Jumatatu.

Vikosi vya usalama vya Somalia vimetangaza kupata mafanikio makubwa katika wiki za hivi karibuni dhidi ya genge la ukufurishaji la al Shabaab limejitangaza kuwa ni tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaeda. Serikali ya Somalia imesema kuwa, imepata mafanikio hayo kwa kupigana bega kwa bega na vikundi vya kujilinda vya kkieneo ambavyo vimechoshwa na jinai na mauaji ya kundi la al Shabaab.

Genge la al Shabaab linaendelea kufanya mashambulizi mabaya, yakiwemo mawili ya Ijumaa iliyopita ambayo yaliua takriban watu 16 na jingine la jana Jumatatu ambalo polisi wamesema limeua watu wasiopungua watano.

Genge la ukufurishaji la al Shabab linafanya jinai kubwa nchini Somalia

 

Ikumbukwe kuwa miripuko miwili ya kigaidi ilitokea jana Jumatatu huko nchini Somalia mbali na kuua watu wasiopungua watano, limejeruhiwa watu wengine kadhaa.

Gavana wa jimbo la Hairan huko Somalia amesema kwamba miripuko hiyo miwili imetokea katika kituo cha kijeshi cha eneo la Baladwain la katikati mwa Somalia..

Genge la kigaidi la al Shabaab limekuwa likijaribu kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007.

Al-Shabaab walifukuzwa Mogadishu na Jeshi la Somalia na vikosi vya Umoja wa Afrika mwaka 2011, hata hivyo, kundi hilo la kigaidi bado linadhibiti maeneo makubwa ya vijijini nchini humo.