Oct 04, 2022 14:03 UTC
  • Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu Uganda afutwa kazi baada ya kutisha kuvamia Kenya

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemuondoa mwanae, Muhoozi Kainerugaba kama Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu masaa machache kufuatia matamshi aliyotoa katika mitandao ya kijamii kuwa ataivamia nchi jirani ya Kenya na kuuteka mji wa Nairobi.

Hatahivyo ingawa Museveni amemfuta kazi Kainerugaba kama kamanda wa jeshi la nchi kavu lakini amepandisha cheo kutoka Luteni Jenerali hadi  Jenerali.

Siku ya Jumatatu Jenerali Kainerugaba aliibua gumzo katika mtandao wa Twitter baada ya kuandika kuwa  jeshi lake linaweza kuuteka mji mkuu wa Kenya, Nairobi katika muda wa wiki mbili. Mtoto huyo wa Museveni aliandika kwenye mtandao wake wa twitter kuhusu kutofurahishwa kwakwe na hatua ya Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, katika uchaguzi wa hivi karibuni, kutogombea kwa muhula wa tatu wa urais, kinyume na katiba ya Kenya.

 

Rais Museveni wa Uganda

Serikali ya Uganda imejibu mjadala wa mitandao ya kijamii ulioibuliwa na Kainerugaba na kusema haifanyi sera za kigeni kwenye mitandao ya kijamii, na kwamba Uganda inathamini uhusiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili na Kenya.

Msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Felix Kulayigye pia amesema Uganda ina uhusiano mzuri na Kenya na hivyo jeshi la Uganda haliwezi kuivamia nchi hiyo jirani.

Jumanne asubuhi, Jenerali Kainerugaba alisema kuwa alizungumza na babake Rais Yoweri Museveni ambaye angetangaza mabadiliko. Wakati huo huo waziri mteule wa mambo ya nje Kenya Alfred Mutua leo amekutana na Balozi wa Uganda Kenya Dr Hassan Galiwango ambapo amesema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kufuatia matamshi ya Jenerali Kainerugaba.