Oct 05, 2022 02:06 UTC
  • Waasi wa M23 wasababisha watoto wengi kukosa elimu Rutshuru DRC

Katika eneo la Rumangabo wilayani Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC mamia ya watoto wanakosa elimu kufuatia mashambulizi na uvamizi wa kundi la wapiganaji wa M23 uliosababisha watu zaidi ya elfu kumi kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao.

Takriban kwa miezi mitatu sasa vijiji vyao viko chini ya udhibiti wa waasi M23 na wao wanapata hifadhi kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani katika kijiji cha Rumangabo kando kando ya mbuga ya wanyama ya Virunga.

Mbali ya watoto kukosa elimu changamoto zingine kubwa zinazowakabili ni ukosefu wa chakula na malazi. Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini DRC nyumba nyingi katika eneo hili ziko katika hali duni na wanakabiliwa na changamoto nyingine za huduma muhimu ikiwemo za usafi.  

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kupitia afisa wake wa mawasiliano bwana Jean-Jacques Simon limesema kuwa tayari wanatoa mafunzo ya elimu mbadala yanayolenga kupunguza ucheleweshaji wa watoto kujifunza shuleni.

Afisa huyo wa UNICEF amesema hayo yote ni kwa sababu UNICEF inaendelea kusaidia licha ya hali ya usalama kuwa ya kutatanisha katika maeneo hayo ambayo watoto wanakimbia kutokana na mzozo ambao unaleta uchungu mkubwa.

Waasi wa M23

Amesema vituo hivyo vya elimu mbadala vinajumuisha ushirikiano wa serekali na wizara ya elimu nchini DRC ni wazi kwamba kutakuwa na mkakati wa kusaidia wanafunzi hao ama kuanzia darasa walilokuwemo kabla ya vita au watapanda daraja sababu walipata elimu wakati wa vita.

Kwa upande wa serikali ya DRC nayo inachukua hatua kwani Gavana wa mkoa wa kivu kaskazini Jenerali Costant Ndima, amesema tayari amewasilisha ripoti kwa serekali kuu na amefanya ziara ya dharura jijini Kinshasa ili kuzungumza na waziri husika wa masuala ya kibinadamu pamoja na shirika la UNICEF ili kuangalia vipi wanaweza kutoa msaada zaidi kwa wathrika hawa pamoja na kwamba tayari UNICEF imeanza kutoa baadhi ya msaada.

Mwezi Agosti wataalamu Umoja wa Mataifa walisema kwamba kuna "ushahidi madhubuti" wa kuthibitisha kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 nchini DRC.

Ripoti hiyo ilikuja baada ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuituhumu Rwanda kila mara kuwa inawasaidia waasi hao wa M23, ambao katika miezi ya karibuni wameyateka maeneo kadhaa ya ardhi ya Kongo. Hata hivyo Rwanda imekuwa ikikanusha kuliunga mkono kundi hilo; na M23 yenyewe imekuwa ikisisitiza kuwa haiungwi mkono wala kupatiwa misaada yoyote na serikali ya Kigali.