Oct 05, 2022 13:09 UTC
  • Kesi tatu za polio zaripotiwa Malawi

Kesi tatu zaidi za polio zimepatikana nchini Malawi na kufanya jumla ya kesi zilizorekodiwa mwaka huu kufikia nne.

Wizara ya Afya ya Malawi imesema kesi hizo tatu mpya zimerekodiwa katika wilaya za kusini mwa Mwanza, Phalombe, na Mulanje zinazopakana na Msumbiji.

Adrian Chikumbe, msemaji wa Wizara ya Afya aliliambia Shirika la Anadolu  Jumanne kwamba, "Wizara hiyo itaongeza juhudi zake za kufuatilia ugonjwa huo.”

Malawi, nchi yenye wakazi wapatao milioni 18.5 kusini mashariki mwa Afrika, ilitangaza mlipuko wa polio mwezi Februari baada ya kisa kimoja kupatikana kwa msichana wa miaka 3 - cha kwanza cha aina hiyo barani Afrika kwa zaidi ya miaka mitano.

Uchambuzi wa kimaabara wakati huo ulionyesha matatizo yaliyogunduliwa nchini Malawi ni sawa naale ya kusini mwa jimbo la Sindh la Pakistani, nchi pekee mbali na Afghanistan ambako polio bado inaenea.

Chikumbe alisema Malawi sasa ina "kazi kubwa" ya kupambana na mlipuko huo ili isiandikwe kama nchi yenye ugonjwa wa polio.

 “Pamoja na hayo, kesi zote zinatoka nje ya nchi; tutahakikisha kwamba hakuna kuenea tena kwa virusi kwa vile havina tiba. Hatutaki kurejea kujulikana kama nchi yenye ugonjwa wa polio,” alisema. Malawi ilipata hali ya kutokuwa na polio mwaka 2005.

Mtoto akipata chanjo ya polio

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kesi zilizoripotiwa mwezi Februari nchini Malawi ni za kwanza barani Afrika katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano.

Kisa cha mwisho cha virusi vya polio barani Afrika kilitambuliwa kaskazini mwa Nigeria mnamo mwaka 2016 na duniani kote kulikuwa na visa vitano tu mwaka jana.

Polio ni ugonjwa unaoambukiza kwa urahisi, ambao huvamia mfumo wa neva na unaweza kusababisha kupooza kabisa mwili ndani ya saa chache. WHO inasema ingawa hakuna tiba ya polio, ugonjwa huo unaweza kuzuiwa kwa kutumia chanjo.