Oct 05, 2022 13:42 UTC
  • Mzozo wapelekea watu milioni moja kukimbia makazi yao Cabo Delgado Msumbiji

Wiki hii wakazi wa Jimbo la Cabo Delgado lililoko kaskazini mwa Msumbiji wanatimiza miaka mitano tangu vurugu kuibuka katika eneo hilo na kusababisha zaidi ya watu milioni moja kuyakimbia makazi yao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR huko Geneva Uswisi, wakazi wa jimbo hilo wameshuhudia madhila makubwa yakitendeka mbele ya macho yao ikiwa ni pamoja na wapendwa wao kuuawa, kukatwa vichwa, kubakwa, nyumba zao na miundombinu mingine kuchomwa moto, huku wanaume na wavulana wakilazimishwa kujiunga na vikundi vya wapiganaji wenye silaha. 

Msemaji wa UNHCR Matthew Saltmarsh amesema “Katika kipindi cha miaka mitano , hali ya kibinadamu imezidi kuwa mbaya katika eneo zima la Cabo Delgado na wakimbizi wa ndani wameongezeka kwa asilimia 20 na kufikia watu 946,508 katika kipindi cha nusu mwaka ya mwaka huu.”

Saltmarsh ameongeza kuwa mzozo huo umeongezeka hadi kufikia maeneo jirani ya majimbo ya Nampula ambapo kumeshuhudiwa matukio manne ya ushambuliaji yaliyofanywa na makundi ya watu wenye silaha mwezi Septemba na kuathiri watu 47,000 na wengine 12,000 kuyakimbia makazi yao.

UNHCR imesema watu waliokimbia makazi yao wana uwoga na wana njaa huku kukiwa na uhaba wa vifaa vya matibabu na sehemu za kutoa malazi zikiwa zimejaa watu hali inayofanya maeneo mengine familia ya watu wanne kukaa ndani ya chumba kimoja.

UNHCR inafanya kazi kwa karibu na serikali na washirika wengine wanaosaidia kutetea wakimbizi wa ndani ili waweze kupata huduma zinazotolewa kitaifa.

Hadi kufikia mwezi Septemba 2022, dola milioni 36.7 zilikuwa zinahitajika ili kuiwezesha UNHCR kutoa huduma na usaidizi wa kuokoa maisha nchini Msumbiji hali ya kuwa fedha zilizopatikana kufikia sasa ni asilimia 60 pekee.