Oct 06, 2022 10:01 UTC
  • Ethiopia na waasi wa TPLF waafiki mazungumzo ya amani

Mazungumzo ya kusaka amani kaskazini mwa Ethiopia yanatazamiwa kuanza baada ya pande hasimu, yaani waasi na serikali kuafiki upatanishi wa Umoja wa Afrika.

Wawakilishi wa Ethiopia na waasi wa kundi la Harakati ya Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) wanatazamiwa kuanza mazungumzo baada ya pande hizo mbili kukubali mwaliko wa Umoja wa Afrika kushiriki katika mazungumzo ya amani yenye lengo la kumaliza mzozo wa miaka miwili.

Mazungumzo hayo yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma hili nchini Afrika Kusini, yatakuwa ya kwanza rasmi, kati ya pande hizo mbili tangu vita vilipozuka Novemba 2020.

Mzozo huo umeua maelfu ya raia na kufanya mamilioni ya watu kuwa wakimbizi. Pande zote mbili hapo awali zilisema zimejiandaa kushiriki katika mazungumzo ya upatanishi yanayosimamiwa na AU lakini mapigano makali yameendelea kushuhudiwa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Serikali ya Ethiopia "imekubali mwaliko huu ambao unaambatana na msimamo wetu wa kanuni kuhusu utatuzi wa amani wa mzozo huo na haja ya kuwa na mazungumzo bila masharti," Redwan Hussein, mshauri wa usalama wa taifa wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed, amesema kwenye Twitter.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed

Katika taarifa waasi wa TPLF wamesema wamekubali mwaliko huo wa mazungumzo ambayo yataongozwa na mwenyekiti wa kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat.

Serikali ya Ethiopia ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed inaituhumu TPLF kwa kujaribu kurejesha utawala wake katika nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika. TPLF iliongoza muungano tawala Ethiopia kwa karibu miaka 30 kabla ya kuondolewa madarakani mwaka 2018 wakati Abiy Ahmed alipoingia madarakani. TPLF inamtuhumu Abiy Ahmed kwa kujiongezea mamlaka na kuwakandamiza Watigray.