Oct 06, 2022 10:09 UTC
  • UN:  Kuna mateso, unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yenye migogoro DRC

Kesi za mateso, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na unyama, zimekithiri katika maeneo yenye migogoro katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hasa kutokana na hali ya kutojali sheria.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (UNJHRO) na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu nchini DR Congo (MONUSCO) ambaye imeangazia matukio ya  kipindi cha kati ya Aprili 1, 2019 na Aprili 30 mwaka huu.

Kulingana na ripoti hiyo, asilimia 93 ya visa 3,618 vilivyosajiliwa vya mateso, ukatili, unyama au udhalilishaji vilivyoathiri wahasiriwa 4,946 vilikuwa katika maeneo yaliyoathiriwa na vita.

Ripoti hiyo imebaini kuwa kesi 492 zilikuwa za ukatili wa kijinsia ambapo watu 761 waliathiriwa. Hali ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, haswa sehemu zake za mashariki, imekuwa tata kwa miongo kadhaa, huku maelfu ya makundi ya waasi wa kigeni na wa ndani yakieneza uhalifu wao katika eneo hilo.

Ripoti hiyo imesema askari wa vikosi vya ulinzi na usalama walibainika kuhusika katika kesi 1,293 kati ya hizo. Ripoti hiyo imeongeza kuwa "licha ya ukubwa wa ukiukaji na unyanyasaji uliofanywa, ni maafisa wawili tu wa jeshi, maafisa wa polisi wa kitaifa 12 na wanachama 75 wa makundi yenye silaha ndio waliopatikana na hatia ya utesaji."

Nada al-Nashif, kaimu kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, alitoa wito kwa mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo "kuchukua hatua kwa uharaka na azma ya kukomesha janga hili." "Mateso hayawezi kamwe kuhesabiwa kuwa haki, bila kujali mazingira."

Naye Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa MONUSCO Bintou Keita amesema, "MONUSCO inaendelea kuunga mkono serikali katika juhudi zake za kuzuia na kupambana na mateso."  

Bintou Keita amesisitiza zaidi kwamba, "kamati za ufuatiliaji wa ukiukaji wa haki za binadamu unaotokana na jeshi la taifa na polisi, iliyoundwa na mamlaka ya kitaifa na kuungwa mkono na MONUSCO, zimeonekana kuwa muhimu katika kusaidia mafunzo katika eneo hili na kuhakikisha ufuatiliaji wa kesi za mateso.”