Oct 06, 2022 13:37 UTC
  • Nigeria: Mateka wa mwisho katika shambulio la treni la mwezi Machi waachiliwa huru

Mateka 23 wa mwisho waliokuwa wakishikiliwa na watu wenye silaha huko Nigeria ambao walitekeleza shambulio kubwa katika treni huko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wameachiwa huru. Hayo yameelezwa na maafisa husika wa nchi hiyo.

Nigeria ambayo inajiandaa kumchagua rais mpya tarehe 25 mwezi Februari mwaka kesho inakabiliwa na mshambulizi ya mara kwa mara ya makundi yanayobebe silaha. Magenge ya uhalifu yamekuwa yakivishambulia vijiji mbalimbali na kuiba ng'ombe za wenyeji wa vijiji hivyo katika maeneo ya kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria. Magenge hayo ya uhalifu pia huwateka nyara maafisa wa serikali na abiria wa kawaida huku wakidai kupewa mlungura. 

Tarehe 28 Machi mwaka huu, watu wanane waliuawa na makumi ya wengine walitekwa nyara wakati watu waliokuwa na silaha waliporipua bomu katika njia ya reli na kuanza kulifyatulia risasi gari moshi lililokuwa likitoka katika mji mkuu, Abuja, kuelekea katika jimbo la Kaduna. 

Miezi sita baada ya shambulio hilo, maafisa wa serikali ya Nigeria walitangaza kuwa wamefanikisha kuachiwa huru wasafiri 23 waliokuwa wakishikiliwa na genge la watekaji nyara. Imebainika kuwa, magenge hayo ya wahalifu kaskazini magharibi mwa Nigeria hufanya hujuma na mashambulizi ili kupata fedha na si kwa sababu za  kiitikadi. Hata hivyo, ushirikiano wa hivi karibuni kati ya majambazi na magenge ya watu wasiojulikana umeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii.

Wananchi wa Nigeria wakitoa wito kwa Rais Buhari 

Baadhi ya duru za usalama zinaamini kuwa wanamgambo hao wenye silaha kutoka kundi la Ansaru lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida lilishirikiana  na magenge mbalimbali ya uhalifu katika hujuma dhidi ya treni huko Abuja mwezi Machi mwaka huu. 

Tags