Oct 07, 2022 02:32 UTC
  • Maafa yanayohusiana na tabianchi yameua watu 150 nchini Rwanda kwa muda wa miezi 9

Takriban watu 150 waliuawa na 300 kujeruhiwa katika maafa yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi nchini Rwanda katika kipindi cha miezi tisa mwaka huu, ripoti ya Wizara ya Usimamizi wa Dharura ilisema Alhamisi.

Maafa hayo yaliyosababisha uharibifu katika maeneo mbalimbali ya Rwanda ni pamoja na mafuriko, maporomoko ya ardhi, dhoruba za upepo na mvua kali miongoni mwa mengine, ripoti hiyo ilisema na kuongeza kuwa matukio 1,033 yalirekodiwa katika kipindi hicho.

Maafa hayo pia yameharibu nyumba 3,378, hekari 1,631 za ardhi za mazao mbali na kusababisha uharibifu katika miundombinu kama vile barabara, madaraja, madarasa na njia za umeme.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na vifo yalikuwa magharibi na kusini mwa Rwanda.

Vifo vilivyosababishwa na majanga viliongezeka kutoka 100 vilivyosajiliwa kati ya Januari na Septemba mwaka jana.

Idadi ya majeruhi, wakati huo huo, ilipanda kutoka 195 iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mnamo 2021.

Mwezi uliopita, Shirika la Hali ya Hewa la Rwanda lilitabiri mafuriko, maporomoko ya ardhi, upepo mkali na matukio mengine mabaya ya hali ya hewa katika baadhi ya maeneo ya nchi katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa mwaka huu, licha ya kupungua kwa mvua.

Maafa baada ya mafuriko Rwanda

Ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa wiki iliyopita ilionya kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinaweza kumomonyoa kati ya 5% na 7% ya Pato la Taifa la Rwanda ifikapo mwaka 2050 ikiwa hazitapunguzwa na kudhibitiwa.

Ripoti ya  Hali ya Tabianchi Rwanda ilionyesha kuwa ingawa nchi hii ndogo ya mashariki mwa Afrika inachangia asilimia 0.003 pekee katika utoaji wa gesi chafuzi duniani, Rwanda iko katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mabadiliko ya hali ya hewa yana uwezekano wa kuongeza tofauti katika mavuno ya mazao na uzalishaji wa kilimo, kusababisha mafuriko makubwa na kupunguza uzalishaji wa nguvu kazi, kulingana na utafiti.