Oct 07, 2022 02:34 UTC
  • Kiwango cha vifo vya watoto chaongezeka mara nne katika eneo la Tigray, Ethiopia

Kiwango cha vifo vya watoto wanaoaga dunia katika mwezi wao wa kwanza wa maisha katika eneo lenye mzozo la Tigray nchini Ethiopia, kimeripotiwa kuwa ni mara nne ya kiwango cha kabla ya vita katika eneo hilo.

Hayo ni matokeo ya utafiti uiliofanyika hivi karibuni katika eneo hilo lililoathiriwa na vita vya ndani nchini Erhiopia.

Awali sababu za kawaida za vifo vya watoto wachanga zilikuwa kuzaliwa kabla ya wakati, maambukizo na ukosefu wa hewa wakati wa kuzaa.

Bereket Berhe, Daktari wa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Ayder anasema: Vifo vya watoto chini ya miaka mitano wakati wa vita vya Tigray viliongezeka maradufu ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya vita. Daktari huyo ameongeza kuwa, vifo vya watoto katika vitengo siku 28 za kwanza za maisha, pia vimeongezeka mara nne katika eneo hilo ikilinganishwa na kabla ya vita.

Takriban miaka miwili imepita tangu vita vianze katika eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia kati ya jeshi la serikali kuu ya nchi hiyo na waasi wa kundi la Harakati ya Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF). Mapigano yanayoendelea katika eneo hilo yamelifanya litengwe na maeneo mengine ya dunia, na kukata huduma za msingi kama vile umeme, simu, mtandao na benki.

Mwezi uliopita wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliionyooshea kidole cha lawama serikali ya Addis Ababa wakisema kuwa, inahusika na vitendo vya uhalifu wa kivita katika eneo la Tigray.

 Katika ripoti yake, Tume ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu nchini Ethiopia iliangazia kile ilichokiita taarifa za kuaminika za mauaji makubwa yaliyofanywa na jeshi la ulinzi la taifa la Ethiopia, ambayo yaliwalenga wanaume na wavulana wa Tigray walio katika umri wa kupigana.

Ripoti hiyo inasema ukiukaji wa haki za binadamu umefanywa na pande zote.

Serikali ya Ethiopia imepinga ripoti ya tume ya Umoja wa Mataifa, na kuielezea kuwa ‘’isiyo kamili, isiyo na msingi na isiyo na uthibitisho’’. 

Wawakilishi wa Ethiopia na waasi wa kundi la Harakati ya Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) wanatazamiwa kuanza mazungumzo baada ya pande hizo mbili kukubali mwaliko wa Umoja wa Afrika kushiriki katika mazungumzo ya amani yenye lengo la kumaliza mzozo wa miaka miwili.