Oct 07, 2022 08:08 UTC
  • WHO: Afrika inaongoza kwa wanaojiua duniani

Shirika la Afya Duniani, WHO, limezindua kampeni mpya ili kuchagiza uelewa na kuchukua hatua kwa ajili ya kuzuia kujiua barani Afrika ambako kuna viwango vikubwa vya vifo vinavyotokana na kujiua.

Kwa mujibu wa takiwimu za shirika hilo zilizotolewa Alhamisi mjini Brazaville, nchini Congo,  karibu watu 11 katika kila watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa kujiua Afrika kikiwa ni kiwango kikubwa zaidi ya kiwango cha wastani cha kimataifa ambacho ni watu 9 kwa kila watu 100,000.

WHO inasema “Hali hii inatokana kwa kiasi kikubwa na kutochukuliwa hatua za kushughulikia na kuzuia sababu za hatari ikiwemo hali ya matatizo ya afya ya akili ambayo kwa sasa inaathiri watu milioni 116 likiwa ni ongezeko kubwa kutoka watu milioni 53 mwaka 1990.”

Kampeni hiyo kupitia mitandao ya kijamii, iliyozinduliwa kabla ya siku ya afya ya akili duniani, inalenga kufikia watu milioni 10 kote kanda ya Afrika ili kuhamasisha umma na kuhamasisha uungwaji mkono wa serikali na watunga sera kwa ajili ya kuongeza umakini na ufadhili wa programu za afya ya akili, pamoja na juhudi za kuzuia watu kujiua.

Dkt.Matshidiso Moeti

Juhudi hizo ni pamoja na kuwawezesha wahudumu wa afya kusaidia zaidi wale wanaokabiliana na fikra za kujiua, kuwaelimisha watu ambao wanaweza kupata fikra hizo juu ya wapi pa kupata usaidizi pamoja na kuhamasisha umma jinsi ya kutambua na kusaidia wale wanaohitaji msaada na kusaidia kukabiliana na unyanyapaa unaohusishwa na afya ya akili na kujiua, kifafa, matatizo ya afya ya akili na matumizi mabaya ya pombe na madawa ya kulevya.

Dkt. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema "Kujiua ni tatizo kubwa la afya ya umma na kila kifo cha kujiua ni janga. Kwa bahati mbaya, hatua za kuzuia kujiua ni mara chache sana kuwa kipaumbele katika programu za afya za kitaifa. Uwekezaji mkubwa lazima ufanywe ili kukabiliana na mzigo unaoongezeka kwa Afrika wa magonjwa sugu na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile matatizo ya akili ambayo yanaweza kuchangia kujiua."