Jan 17, 2018 14:53 UTC
  • Sisitizo la Sudan, Kodivaa, Gambia na Morocco la kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu

Wawakilishi wa nchi za Kiafrika za Sudan, Kodivaa, Gambia na Morocco wamesisitiza katika Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu (OIC) kupatiwa ufumbuzi matatizo yanayoukabili Ulimwengu wa Kiislamu na kukabiliana pia na utawala ghasibu za Kizayuni.

Aisha Muhammad Ahmad Saleh Naibu Spika wa Bunge la Sudan ameashiria leo katika siku ya pili ya Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Kiislamu Wanachama wa OIC hapa Tehran kuhusu changamoto zinazoukabili Ulimwengu wa Kiislamu na kueleza kuwa wananchi wa Palestina wanakabiliwa na hali mbaya huku maghasibu wakiitangaza Beitul Muqaddas ambao ni mji mkuu wa Waislamu duniani kote kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni. 

Naibu Spika wa bunge la Sudan ameeleza kuwa machafuko na vitendo vya kigaidi havina uhusiano wowote na Uislamu na kwamba Marekani ndio chimbuko la tatizo hili. Amesema kwa msingi huo maamuzi ya dhati yanapasa kuchukuliwa ili kutokomeza chimbuko la ugaidi ili umma wa Kiislamu uwe na mshikamamo wa kutosha. 

Naye Joelad Privatola Naibu Spika wa Bunge la Kodivaa amesisitiza kuwa kadhia ya Palestina ni miongoni mwa masuala makuu ya Ulimwengu wa Kiislamu na kwamba kikao cha Tehran kimebainisha msimamo wa wazi kuhusu kadhia ya Palestina na kutaka kuchukuliwa hatua kuhusu suala hilo.  Naibu Spika wa bunge la Kodivaa amesisitiza pia kuhusu kuheshimiwa haki za wanawake na kushughulikiwa hali zao na kubainisha kuwa: Kuna haja ya kuundwa kamati ya kisheria itakayoshughulikia utekelezaji wa maazimio kwa shabaha ya kuboresha hali ya wanawake. 

Momodou Sanneh Naibu Spika wa Bunge la Gambia pia amesisitiza katika siku ya pili ya Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu Wanachama wa OIC unaofanyika hapa Tehran kuwa nchi za Kiislamu zinapasa kuchukua hatua za pamoja za kustawisha na kuimarisha suhula za pamoja na kwamba changamoto mbalimbali zinazoukabili hii leo Ulimwengu wa Kiislamu kama umaskini, ukiukaji wa haki za binadamu, mizozo na ugaidi zinaweza kutatuliwa kwa njia ya kirafiki na amani. 

Momodou Sanneh, Naibu Spika wa Bunge la Gambia
 

Wakati huo huo Abdulwahid al Ansari Naibu Spika wa Bunge la Morocco ameitaja kadhia ya Palestina kuwa suala linaloziunganisha nchi zote za Kiislamu na kueleza kuwa nchi zote za Kiislamu zinapasa kushikamana na kuwa kitu kimoja kuhusu Quds na kadhia ya Palestina ili Marekani iheshimu haki za wananchi wa Palestina. 

  

Tags

Maoni