Apr 03, 2018 11:54 UTC
  • Sisitizo la Iran juu ya udharura wa kuchukuliwa hatua za maana za upokonyaji silaha za nyuklia

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa hotuba mbele ya kamati ya upokonyaji silaha na usalama wa kimataifa ya umoja huo na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za maana kwa ajili ya upokonyaji silaha za nyuklia.

Gholamali Khoshroo amesisitiza kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kivitendo kwa ajili ya kuanzisha eneo lisilo na silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati. Balozi na mwakilishi huyo wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisema hayo Jumatatu ya jana katika kikao cha mwaka huu cha Kamisheni ya Upokonyaji Silaha ya Umoja wa Mataifa huko mjini New York ambapo sambamba na kuashiria hatua za Marekani za kukiuka makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA amebainisha kwamba, makubaliano hayo sio kitu cha upande mmoja, bali wajumbe wengine wa makubaliano hayo nao wanapaswa kutekeleza kivitendo wajibu wao.

Ukweli ni kuwa kwa sasa suala la upokonyaji silaha linakabiliwa na changamoto muhimu ambayo ni ujadidishaji wa silaha za nyuklia na kuendelea mashindano ya silaha hizo baina ya madola yaliyonazo ambapo mwenendo huu kwa hakika ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa dunia. Marekani ikiwa moja ya madola makubwa yenye kumiliki silaha za atomiki, mwaka 1945 iliishambulia kwa mabomu ya atomiki miji ya Horoshima na Nagasaki huko Japan na kuwaua maelfu ya watu na kuacha athari nyingi haribifu kwa mazingira. Hivi sasa Marekani imeliweka katika mipango yake suala la kujadidisha na kuzifanya za kisasa silaha zake kongwe za nyuklia na kuzalisha kizazi kipya cha silaha hizo angamizi mikakati ambayo haina maana nyingine bighari ya kueneza silaha za nyuklia.

Noam Chomsky, mchambuzi na mnadharia wa Kimarekani

Kwa muktadha huo, madai ya Marekani kwamba ina wasiwasi na suala la kuenea silaha za nyuklia ni kichekesho na ni katika mwendelezo wa siasa zake za hadaa. Noam Chomsky, mchambuzi na mwananadharia wa Kimarekani amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Euro News kuwa, Marekani na Israel ndio vyanzo vikuu vya tishio la nyuklia katika Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima kwa ujumla. Chomsky amesema bayana kwamba: "...Uchunguzi wa maoni wa kimataifa uliofanywa na mashirika ya uchunguzi wa maoni ya Marekani unaonyesha kuwa, akthari ya wananchi wa mataifa ya dunia wanaitaja Marekani kuwa, hatari na tishio kubwa zaidi kwa amani ya dunia."

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwamba, mpango wa kulisafisha eneo la Mashariki ya Kati na silaha za atomiki hadi sasa haujafanikiwa kutokana na siasa za kupenda vita za utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa:

Suala la kuulazimisha utawala wa Kizayuni wa Israel ujiunge na mpango wa kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia (NPT) na kuzifanya shughuli na taasisi zake ziwe chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) inapasa liwe moja ya nasaha na maelekezo makuu ya kamisheni ya upokonyaji silaha.

Nagasaki

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kidhahiri anaonekana kuchukua hatua za kimsingi kwa ajili ya kufanyika mazungumzo ya upokonyaji silaha. Marc Finaud mtaalamu wa kituo cha Geneva kwa ajili ya sera za kiusalama anaamini kwamba, kuna uwezekano Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akatumia azimio nambari 1887 la Baraza la Usalama kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la mpango alionao wa kutekeleza upokonyaji silaha za atomiki ulimwenguni.

Azimio nambari 1887 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilipasishwa Septemba 24 mwaka 2009 na wanachama wote wa baraza hilo ni hati ya kimataifa inayohusu kulinda amani na usalama wa kimataifa na inayopinga kueneza silaha za atomiki na wakati huo huo kutaka ufanyike upokonyaji wa silaha hizo hatari. Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ili kufikiwa kikamilifu malengo ya upokonyaji silaha za atomiki kuna haja ya kuweko azma thabiti ya kuangamiza silaha zote hizo.

Katika mkutano uliofanyika Aprili mwaka 2011 mjini Tehran kuhusiana na suala la upokonyaji silaha, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema bayana katika sehemu moja ya ujumbe wake kwa mkutano huo wa kimataifa kwamba: "Sisi tunaitakidi kuwa ni haramu kutumia silaha hizi na tunaamini kwamba, ni jukumu la watu wote kufanya juhudi kwa ajili ya kuilinda jamii ya mwanadamu na balaa hili kubwa."