Mar 21, 2019 15:43 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Iran itawapiga mweleka maadui katika vita vya kiuchumi dhidi ya taifa hili

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwaka mpya wa Kiirani unaoanza hii leo utakuwa mwaka wa fursa kubwa na wala hautakuwa wa vitisho kama wanavyodai wengine, na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itamshinda adui katika vita vyake vya kiuchumi dhidi ya taifa hili.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo hii leo wakati akihutubia umati mkubwa wa watu katika Haram ya Imam Ridha AS katika mji mtakatifu wa Mashhad ulioko kaskazini mashariki mwa nchi na kuongeza kuwa: "Tunaweza kuvigeuza vikwazo kuwa fursa. Hivi sasa kila mmoja anatambua kuwa adui anachochea vita vya kiuchumi, kisiasa na kiintelijensia dhidi ya Iran, lakini kwa uwezo wa Allah tutamshinda adui."

Amebainisha kuwa, "Tunapaswa kufika pahala ambapo maadui waelewe kwamba vita vya kiuchumi haviwezi kulidhuru au kuliweka chini ya mashinikizo taifa la Iran. Naamini kwamba mwaka huu mpya wa Kiirani utakuwa mwaka wa fursa na mwaka ambao changamoto zote zitapatiwa ufumbuzi."

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuimarisha uwezo wake wa kujihami, licha ya mashinikizo ya maadui.

Ameashiria vikwazo ilivyowekewa Iran katika vita vya Iraq dhidi ya nchi hii katika miaka ya 1980 na kusema kuwa, "Hakuna nchi hata moja iliyoipa Iran japo nyaya za kutengeneza uzio ili kujilinda, lakini vijana wa Kiiarani waliweza kutoa jibu kali kwa waanzilishi wa vita hivyo." 

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa pongezi, kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali AS, Imam wa kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akihutubia hadhirina katika Haram ya Imam Ridha AS mjini Mashhad

Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 13 Rajab, miaka 1463 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, ambapo mwaka huu ilisadifiana na tarehe ya jana Jumatano.

Wakati huohuo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezikosoa vikali nchi za Ulaya kwa kukataa kulitaja shambulizi la hivi karibuni la New Zealand kama hujuma ya kigaidi. Waislamu 50 waliuawa shahidi huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mashambulio hayo dhidi ya misikiti miwili katika mji wa Christchurch nchini New Zealand Ijumaa iliyopita.

Hali kadhalika Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria kutokuwa na muamana nchi za Magharibi na kufafanua kuwa, "Umoja wa Ulaya ulipaswa kusimama kidete dhidi ya hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini ulifeli katika hilo. Nchi za Ulaya zililichoma kisu mgongoni kwa kulisaliti taifa la Iran kwenye makubaliano hayo. Iran haipaswi kuziamini tena nchi hizo kwa kuwa zilishindwa kuonesha kuwa zina muamana au zinaweza kusaidia."

Hadhirina wakifuatilia kwa makini hotuba ya Ayatullah Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mwaka mpya wa Kiirani wa 1398 kuwa mwaka wa "kustawi uzalishaji".

 

 

Tags