Mar 22, 2019 16:58 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Katika kadhia ya JCPOA, Wazungu wametupiga jambia kwa nyuma

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia, jana Alkhamisi jioni alitoa hotuba muhimu sana iliyozingatia masuala mbalimbali Ukiwemo msimamo wa Wamagharibi kuhusu Iran mbele ya mjumuiko mkubwa na uliojaa hamasa wa wafanyaziara na majiran wa Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash'had kaskazini mashariki mwa Iran.

Moja ya jambo muhimu lililofanywa na Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake hiyo ni kuchora ramani na muongozo wa kuweza taifa la Iran kufikia kwenye uwezo mkubwa wa kiuchumi usiotetereka. Amesema lengo hilo la kiistratijia haliwezi kufikiwa ila kwa kutokuwa na tamaa kabisa na msaada wa Wamagharibi. Katika sehemu moja ya hotuba yake hiyo amesema: Uzoefu wa kihistoria na ushahidi wa wazi wa vitendo vya Wamagharibi unaonesha kuwa mtu anaweza kutarajia kutoka kwao njama, usaliti na kushambulia kwa nyuma lakini hawezi kutegemea kutoka kwao urafiki na ushirikiano wa kweli. 

Jambo jingine muhimu lililosisitizwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo ya jana Alkhamisi ni masuala ya Jamhuri ya Kiislamu na serikali za Magharibi. Amesema, watu ambao muda wote wanatoa vitisho kwa taifa, watambue kuwa kutaka na kukataa wameathiriwa na majigambgo na vita vya kisaikolojia vya maadui wa Iran. Kwa ajili ya kuthibitisha hilo ametoa mifano kadhaa ya majigambo ya maadui katika mwaka ulioisha wa 1397 Hijria Shamsia akisema: Mmoja wa wapumbavu daraja moja wa Kimarekani aliwahi kusema kwamba kama watajitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, basi wananchi wa Iran watashindwa hata kununua mkate wa kula na watamiminika barabarani kufanya uasi, kama ambavyo mpumbavu mwingine wa Kimarekani naye alidai kwamba eti sherehe za X-Mass za mwaka 2019 wangelizifanyia mjini Tehran. Kusema kweli maneno hayo ima yanatokana na ujinga na upumbavu wao au pengine ni vita vya kisaikolojia. 

Ikumbukwe kuwa taasisi nyingi za utafiti na za kiistratijia za Marekani zinaamini kwamba kuendesha vita vya kutumia silaha dhidi ya Iran hakuna faida na baya zaidi ni kwamba iwapo Marekani itaanzisha vita vya namna hiyo haitapata matunda mengine isipokuwa vita visivyo na mwisho na kamwe haitopata ushindi kwenye vita hivyo.

Mc Balmer, mmoja wa wanastratijia maarufu wa Kimarekani ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa wabunifu wakubwa wa sera za kisiasa nje ya Marekani anasema: Iran hivi sasa imebadilika na kuwa dola lenye nguvu za kipekee na haiwezekani kuivamia kijeshi na kuanzisha vita vya silaha dhidi yake. Hivyo njia pekee iliyobakia ya kuweza kuupindua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini humo ni kutumia vita laini na taktiki za operesheni za kisaikolojia za kipropaganda yaani kutumia vita vya vyombo vya habari. 

Ni jambo lisilo na shaka kwamba siasa na nguvu za nchi za Magharibi, iwe za Ulaya au Marekani zote zimesimama juu ya msingi wa dhulma, ubeberu, misimamo isiyo ya kimantiki na kupenda kujikumbizia kila kitu upande wao. Vitendo hivyo vya kinafiki na vya nyuso mbili vya nchi za Magharibi vinaonekana wazi zaidi katika masuala ya ugaidi na madai ya kutetea haki za binadamu na suala zima la haki ya mataifa ya dunia ya kufaidika na teknolojia ya nyuklia.

Katika hotuba yake muhimu ya jana Alkhamisi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliligusia suala hilo kwa kusema: Utawala wa Saudi Arabia ndio utawala mbaya kabisa katika eneo hili, ni utawala wa kiimla, kidikteta, dhalimu, fasidi na tegemezi. Hata hivyo nchi za Magharibi zinaupa utawala kama huo suhula za nyuklia na vituo vya kuzalisha makombora kwani ni kibaraka wao. Tukizingatia uhakika huo tutaona kuwa, ushari na ushetani ndiyo dhati ya nchi za Ulaya na Marekani.

Sehemu ya umati mkubwa wa watu wakisikiliza hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Haram ya Imam Ridha AS huko Mash'had, Machi 21, 2019

Amma kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, baina ya ahadi zilizotolewa na Ulaya kuhusu mapatano hayo na vitendo vya nchi hizo kwa Iran kuna tofauti kubwa ya baina ya mbingu na ardhi. Kiongozi Muadhamu ametilia mkazo jambo hilo kwa kuashiria jinsi nchi za Ulaya zilivyoshindwa kutekeleza ahadi zao kuhusu kuanzisha kanali maalumu ya mabadilishano ya kifedha baina ya Iran na Ulaya. 

Kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu, mafanikio ya kiuchumi ya taifa la Iran yatapatikana kwa kutegemea nguvu za ndani na kutokuwa kabisa na tamaa ya msaada wa madola ya Magharibi na ndio maana ameutaja mwaka huu wa 1398 Hijria Shamsia kuwa ni mwaka wa fursa nyingi za kufanikishia jambo hilo. Vile vile amesisitiza kuwa: Uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya ulinzi kwa hakika umefikia daraja ya kuzuia kushambuliwa kabisa, na nguvu hizo zimepatikana katikati ya vikwazo, hivyo katika masuala ya kiuchumi pia inawezekana kutumia fursa ya vikwazo kulifanya taifa la Iran liwe na nguvu kubwa za kujihami kiuchumi kama ilivyo kwa nguvu zake za kiulinzi.

Tags