Apr 22, 2019 15:06 UTC
  • Rouhani: Iran na Pakistan zimeamua kuunda kikosi cha pamoja cha radiamali ya haraka mpakani mwao

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran na Islamabad zimekubaliana kuunda kikosi cha pamoja cha radiamali ya haraka cha kupambana na ugaidi katika mpaka wao wa pamoja.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo katika mazungumzo na waandishi wa habari aliyoyafanya kwa pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, nchi hizi mbili zimekubaliana kuongeza ushirikiano wao katika masuala ya kiulinzi na kiusalama.

Vile vile amesema mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Pakistan ni hatua mpya katika uhusiano wa Tehran na Islamabad na kufafanua zaidi kwa kusema, nchi hizi mbili zina nia ya kweli ya kustawisha uhusiano baina yao na hakuna nchi yoyote ya tatu inayoweza kutia doa uhusiano wa nchi hizi mbili ndugu jirani.

Aidha amesema, Iran iko tayari kuidhaminia Pakistan mahitaji yake ya nishati kama vile gesi na mafuta na imeshachukua hatua zinazotakiwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Iran kuelekea Pakistan.

Pakistan ni moja ya majirani muhimu wa Iran upande wa kusini mashariki mwa nchi

 

Kwa upande wake, Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan amegusia nafasi muhimu ya Iran katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, Tehran na Islamabad zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kuleta utulivu na amani nchini Afghanistan.

Waziri Mkuu huyo wa Pakistan amesema kuwa, kitendo cha Marekani cha kutambua rasmi milima ya Golan ya Syria kuwa eti ni mali ya utawala wa Kizayuni wa Israel ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa na za haki za binadamu. 

Amezungumzia pia kadhia ya Kashmir na kusisitiza kuwa, mgogoro wa Kashmir hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi hivyo amezitaka Iran na Pakistan kuimarisha uhusiano wao zaidi katika nyanja zote.

Tags

Maoni