Jun 05, 2019 11:42 UTC
  • Rouhani: Iran inafanya juhudi za kuimarisha usalama wa Asia Magharibi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inafanya juhudi za kuimarisha usalama katika eneo la Asia Magharibi na haina hamu wala nia yoyote ya kuingia vitani na nchi nyingine.

Rais Rouhani amesema hayo leo Jumatano katika mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani na huku akimpa mkono wa baraka za Idul Fitr amesema, kama nchi yoyote itachukua hatua isiyo ya busara dhidi ya Iran, bila ya shaka yoyote Jamhuri ya Kiislamu itatoa majibu makali yatakayomfanya adui huyo ajute.

Vile vile amesisitiza kuwa, masuala na matatizo ya eneo hili hayawezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi na kubainisha kwamba: msimamo wa Iran siku zote ni mmoja; kwa maana kwamba, msimamo iliouchukua Tehran wakati dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein alipoivamia Kuwait ndio huo huo ilio nao hivi sasa kuhusu mashambulizi ya Saudia na Imarati huko Yemen na kuhusu vikwazo vya kila upande vya nchi nne za Kiarabu za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri dhidi ya Qatar.

Nchi nne za Kiarabu za Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zimeiwekea vikwazo vya kila upande Qatar. Njia pekee iliyoiokoa Doha ni uhusiano wake mzuri na Iran

Vile vile amesema, siasa za Tehran ni za kustawisha uhusiano wake na Doha na ameisifu Qatar kwa msimamo wake mzuri katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kusema kuwa, siasa hizo zinatokana na ujirani mwema. Aidha amesema, Saudia na Imarati hazina misimamo mizuri kuhusu Iraq, Yemen na Qatar jambo ambalo amesema ni kwa madhara ya eneo hili zima.

Kwa upande wake, Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani naye ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr na kusema kuwa uhusiano wa Iran na nchi yake ni wa kihistoria. Vile vile ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msimamo wake wa kuwa pamoja na Qatar katika kukabiliana na vikwazo vya nchi nne za Kiarabu za Saudia, Imarati, Bahrain na Misri dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu na kusema kuwa, Doha kamwe haitosahau msimamo huo mzuri wa Tehran.

Tags