Jun 05, 2019 11:55 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Nchi za Kiislamu zipambane na adui ghasibu anayetenda jinai Palestina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, nchi za Kiislamu zina wajibu wa kukabiliana na adui ghasibu anayetenda jinai huko Palestina na sio kuzozana zenyewe kwa zenyewe.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatano wakati alipoonana na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu na matabaka mbalimbali ya wananchi hapa mjini Tehran. 

Kiongozi Muadhamu ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwenguni kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr na kusisitiza kuwa kadhia ya Palestina ni suala kuu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa na amezilaumu zile nchi za Kiislamu ambazo zinashiriki katika ufanikishaji wa malengo haramu ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mkutano wa leo wa Kiongozi wa Kiislamu na maafisa wa Serikali

 

Ayatullah Khamenei amesema: Mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ni tofauti na mtazamo wa baadhi ya viongozi wa zamani wa Kiarabu ambao walikuwa wakiamini kuwa lazima Mayahudi watupwe baharini, bali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwanzo kabisa ilikuwa inasisitiza kulindwa taifa la Paletsina na itaendelea kusimama imara kukabiliana na ulimwengu wa kiistikbari. (Ikumbukwe kuwa kuna tofauti baina ya Mayahudi na Wazayuni kwani Mayahudi na Wakristo ni sehemu ya wakazi wa Palestina kama walivyo Waislamu tofauti na Wazayuni).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia pia pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu la kufanyika kura ya maoni itakayowashirikisha wakazi wote wa Palestina; Waislamu, Wakristo na Mayahudi pamoja na wakimbizi wa Kipalestina ili wenyewe waamue ni mfumo wa aina gani wanataka utawale huko Palestina.

Aidha amesema, mapambano ya kijeshi, kisiasa na kiutamaduni ya Wapaletina lazima yaendelee hadi pale wavamizi na maghasibu wa Kizayuni watakapoheshimu maamuzi ya taifa la Palestina.

Tags