Aug 08, 2019 12:31 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Iran: Marekani ndio chanzo hasa cha kukosekana amani katika eneo

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, muungano wa kijeshi unaotaka kuundwa na Marekani wa kisingizio cha kudhamini usalama wa vyombo vya majini ndio utakaosababisha kuvurugika zaidi amani na usalama katika eneo.

Brigedia Jenerali Amir Hatami ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na mawaziri wa ulinzi wa Qatar, Kuwait na Oman.

Katika mazungumzo hayo, Brigedia Jenerali Hatami amesisitiza kuwa, Marekani ndio chanza hasa cha kukosekana amani katika eneo na akabainisha kwamba, usalama wa eneo ni suala la pamoja la Iran na nchi jirani za Ghuba ya Uajemi na kwamba inapasa nchi za eneo hili zifanye mazungumzo athirifu na yenye malengo chanya juu ya suala hilo.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema, kustawisha uhusiano na majirani ni katika misingi mikuu ya sera za nje na ulinzi za Jamhuri ya Kiislamu na akafafanua kwamba: Kukosekana amani katika nchi yoyote au dhidi ya nchi yoyote ya eneo ni jambo lisilokubalika kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na eneo hili halipasi kuwa mahali pa kujifaragua na kujikita madola ajinabi.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri Mshauri wa Masuala ya Ulinzi wa Qatar, Khalid bin Muhammad bin Abdullah al Atiyyah amesisitiza kuwa: Usalama wa eneo inapasa udhaminiwe na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya nchi muhimu sana kwa ajili ya kulinda na kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi.

Sheikh Nasir Sabah al-Ahmad As-Sabah, Naibu wa kwanza wa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Kuwait, yeye amebainisha hamu ya kutaka kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili na kueleza kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu sana na athirifu katika kudumisha amani na uthabiti wa eneo.

Waziri wa Ulinzi wa Oman, Badr bin Saud bin Harib al-Busaidi, yeye ametilia mkazo ulazima wa kushiriki nchi za eneo katika kulinda usalama wa maji ya eneo hili na kuendelezwa mashauriano na ushirikiano wa karibu baina ya nchi mbili hususan vikosi vya wanamaji wa Iran na Oman kwa ajili ya kulinda usalama wa Lango Bahari la Hormuz.../

Tags