Sep 07, 2019 12:58 UTC
  • Kamalvandi: Mashinepewa (centrifuges) za kisasa za nyuklia za Iran zaanza kufanya kazi + Video

Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kuwa, awamu ya tatu ya kupunguza Iran kutekeleza ahadi zake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA ilianza jana Ijumaa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran akisema hayo leo mbele ya waandishi wa habari na huku akitoa ufafanuzi kuhusu vipengee vya awamu hiyo ya tatu amesema kuwa, taasisi hiyo ina jukumu la kuanzisha harakati za kielimu na utafiti wa nyuklia kwa kasi kubwa na bila ya kujifunga na mipaka iliyokuwa imewekwa na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Hatua hiyo ya Iran imechukuliwa baada ya nchi za Ulaya kushindwa kutekeleza ahadi zako ndani ya makubaliano hayo ya kimataifa.

 

Pamoja na hayo Kamalvandi amesema, Iran itaendelea kuwa muwazi kikamilifu katika shughuli zake za nyuklia kama ilivyokuwa huko nyuma. Ameongeza kuwa, mabadiliko haya ya hivi sasa katika utafiti na upanuzi wa shughuli za nyuklia, yataongeza kasi kuelekea kwenye kufikia Iran kiwango cha SEW milioni moja.

Msemaji huyo wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amezungumzia pia hatua nne ambazo zimechukuliwa leo na Iran katika kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA na kufafanua kuwa, hatua ya kwanza inahusiana na kifungu nambari 39 kinachohusiana na kuzalisha bidhaa za urutubishaji urani na mashine za kizazi kipya. Amesisitiza kuwa, leo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umeelezwa kwamba uzalishaji wa bidhaa za utafiti utaongezwa katika akiba ya Iran.

 

Katika upande mwingine, hisia mbalimbali zimeoneshwa duniani kuhusu hatua hii ya Iran ya kuanza kutekeleza kivitendo awamu ya tatu ya kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA, huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akishindwa kuzuia hamaki zake na kupayuka akisema: huu si wakati wa kufanya mazungumzo na Iran ni wakati wa vikwazo tu.

Upayukaji huo wa Waziri Mkuu wa Israel umekuja katika hali ambayo kwa zaidi ya miongo minne sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikipambana kiume na vikwazo vya kila upande vya mabeberu na kwa hakika ni upayukaji kusema kuwa huu ni wakati wa vikwazo tu dhidi ya Iran, wakati muda wote mabeberu na waistakbari wamekuwa wakitumia kila fursa wanayopata kulifanyia uadui na kuliwekea vikwazo taifa la Kiislamu la Iran na hakuna siku ambapo vikwazo hivyo vimeondolewa.

Tags

Maoni