Sep 10, 2019 07:25 UTC
  • Zarif: Israel, mwana kilizi, ndiye mmiliki halisi wa silaha za nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu matamshi ya kijuba ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, aliyedai kuwa ana ushahidi mpya unaoonesha kuwa Tehran inaunda kwa siri silaha za nyuklia; ambapo amesema kauli hiyo ya kichochezi ya Benjamin Netanyahu inalenga kufanikisha ajenda ya vita ya utawala huo haramu.

Muhammad Javad Zarif amesema katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, "Mmiliki halisi wa silaha za nyuklia analia tena. Kwa kutumia madai bandia ya kituo cha Iran kilichoharibiwa, anataka kuhahalisha na kutafuta kisingizio cha kuingia vitani."

Dakta Zarif ameuambatanisha ujumbe huo na picha ya ukurasa wa mbele wa gazeti la Sunday Times la Marekani toleo la Oktoba 5 1986 ambalo liliandika kwa kina habari iliyofichua namna utawala huo ghasibu unaunda silaha za nyuklia.

Amesema Netanyahu na Timu B hawana jingine wanalotaka ghairi ya vita, bila kujali umwagikaji wa damu za watu wasio na hatia, na wako tayari kutumia matrilioni ya dola kufanikisha azma hiyo.

 

Ujumbe wa Zarif kwenye Twitter

Jana Jumatatu Netanyahu bila kutoa ushahidi wowote, aliendeleza wimbi la bwabwaja zake ambapo alidai kuwa Iran imeharibu kituo chake cha kuzalisha silaha za nyuklia kusini mwa mji wa Isfahan, eti baada ya maajenti wa utawala huo khabithi kugundua shughuli hizo.

Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya SIPRI yenye makao yake mjini Stockholm Sweden, inakadiriwa kuwa nchi tisa zinazomiliki silaha za nyuklia duniani yaani Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, utawala wa Kizayuni wa Israel na Korea Kaskazini mwanzoni mwa mwaka huu wa 2019 zilikuwa na silaha za nyuklia karibu 13,865.

Tags

Maoni