Sep 10, 2019 10:39 UTC
  • Muhuri wa IAEA wa kuunga mkono makubaliano ya JCPOA na mchezo mpya wa maigizo wa Netanyahu

Baada ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia (IAEA) kutoa ripoti yake mpya inayotathmini hatua za Iran katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ameibuka tena na kudai kuwa, miradi ya nyuklia ya Iran ni ya kijeshi na kwamba, eti taifa hili linataka kutengeza bomu la atomiki.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akitoa majibu yake kwa madai ya kukaririwa na yasiyo hata na chembe ya ukweli ya Benjamin Netanyahu, aliandika jana Jumatatu katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Mmiliki halisi wa silaha za nyuklia analia tena. Kwa kutumia madai bandia ya kituo cha Iran kilichoharibiwa, anataka kuhahalisha na kutafuta kisingizio cha kuingia vitani."

Dakta Muhammad Javad Zarif alisema, Netanyahu na Timu B hawana jingine wanalotaka ghairi ya vita, bila kujali umwagikaji wa damu za watu wasio na hatia, na wako tayari kutumia matrilioni ya dola kufanikisha azma yao hiyo.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kila mara asasi zinazohusika na miradi ya nyuklia  zinapotangaza kuwa, miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika katika fremu ya malengo ya amani, Benjamin Netanyahu huibuka na kuja na mchezo mpya wa maigizo sambamba na kutoa madai ya kurariri akifanya juhudi za kuziathiri fikra za waliowengi ulimwengu kwa madai yake hayo yasiyo na mashiko.

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Madai ya uongo ya Netanyahui yalikuwa na nafasi muhimu mno katika kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Hadi sasa Waziri Mkuu wa Israel amefanya juhudi kubwa akitumia madai matupu ili kuifanya jamii ya kimataifa iwe pamoja naye dhidi ya Iran. Hata hivyo hadi sasa juhudi zake hizo zimekwaa kisiki.

Tajiriba na uzoefu mchungu wa historia unathibitisha kwamba, mashmbulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003 ambayo yalifanyika kwa kutegemea uongo wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ni kwa kiasi gani yaliteketeza roho za maelfu ya Wairaqi wasio na hatia. Wakati huo Netanyahu akihutubia katika Kongresi ya Marekani 2002 aliishajiisha Washington akitumia madai ya uongo ili iishambulie Iraq kwa kisingizio cha utawala wa Baath wa Saddam Hussein kumiliki silaha za atomiki.

Mashambulio ya Marekani dhidi ya Iraq na kuthibitika kuwa ni uongo kisingizio kilichotumiwa kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu hayakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuteketeza roho za maelfu ya Wairaqi na kuhairibu kabisa miundomsingi ya nchi hiyo ambapo matokeo mabaya ya vita hivyo yangali yanashuhudiwa hadi leo.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

Kuingia madarakani Rais Donald Trump kwa mara nyingine tena kulimuandalia uwanja Benjamin Netanyahu wa kuendelea kupiga ngoma yake hiyo ya vita mara hii dhidi ya Iran. Hata hivyo Netanyahu na timu B wamekumbwa na mkwamo. Hilo ndilo lililomfanya Waziri Mkuu huyo wa Israel aanze kutunga uongo usio na msingi ili kuziwafanya fikra za waliowengi katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla ziwe na mtazamo hasi dhidi ya Iran. Hii ni katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio mmiliki halisi wa silaha za nyuklia katika eneo hili la Asia Magharibi. Israel inamiliki mamia ya vichwa vya nyuklia na katu haiko tayari kuwajibika mbele ya asasi yoyote ile ya kimataifa. Pamoja na hayo Marekani imeendelea kuukingia kifua utawala huo.

Katika uwanja uwanja huo, jana Jumatatu, Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliandika ujumbe mwingine katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuambatanisha  ujumbe huo na picha ya ukurasa wa mbele wa gazeti la Sunday Times la Marekani toleo la Oktoba 5 1986 ambalo liliandika kwa kina habari iliyofichua namna utawala huo ghasibu unavyotengeneza silaha za nyuklia na kuandika kuwa, kituo cha nyuklia cha Israel kimejengwa katika kina cha jangwa na Naqab na kinafanya shughuli zake kwa siri.

Rais Donald Trump wa Marekani

Israel ikisaidiwa na Marekani imeendelea na shughuli zake za miradi ya nyuklia yenye malengo ya kijeshi na vichwa vya nyuklia vya utawala huo ghasibu ni tishio kubwa kwa usalama wa Asia Magharibi na ulimwengu kwa ujumla. Katika mazingira kama haya, madai ya Waziri Mkuu wa Israel dhidi ya Iran ni kioja na kuzidhihaki pamoja na kuzichezeaa shere sheria na asasi za kimataifa ambazo zimeunyamazia kimya au asasi ambazo ni butu na zisizo na utendaji wowote wa maana mbele ya utawala huo hatari na unaopenda vita.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiheshimu sheria za kimataifa ilitia saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuwadhihirishia walimwengu kwamba, yenyewe haina mpango wa kutumia miradi yake ya nyuklia kwa malengo ya kijeshi. Ripoti ya jana Jumatatu ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), kwa mara nyingine tena imethibitisha kuwa, Iran imefungamana kikamilifu namakubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hivyo kuipigia muhuri wa kuunga mkono kwamba, shughuli za nyuklia za Tehran zinafanyika kwa malengo ya amani.

Tags

Maoni