Sep 12, 2019 04:06 UTC
  • Zarif akosoa tangazo la kushadidishwa ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa tangazo la kushadidishwa ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Kiu cha vita kinapaswa kuondoka pamoja na mpenda vita mkuu ."

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake binafsi wa Twitter Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif aliandika: "Katika hali ambayo dunia imepata ahueni, isipokuwa wapenda vita wengine wawili au watatu walioingiwa na kiwewe, baada ya kutimuliwa kinara wa Timu B kutoka Ikulu ya White House, Pompeo na Mnuchin wametangaza kushadidisha vita vya kiuchumi dhidi ya Iran."

Ikumbukwe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo na waziri mwenzake wa fedha Steven  Mnuchin, Jumanne wakiwa katika kikao cha pamoja cha waandishi habari mjini Washington walitangaza kuwa, Wizara ya Fedha ya Marekani itawawekea vikwazo makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

John Bolton aliyetimuliwa kama mshauri wa usalama wa taifa wa Rais Trump wa Marekani

Tangazo hilo limekuja katika hali ambayo mapema Jumanne, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kumfuta kazi mshauri wake wa usalama wa Taifa John Bolton, ambaye alikuwa maarufu kwa mitazamo yake ya kupenda vita hasa kuchochea Iran ishambuliwe kijeshi.

Huko nyuma Zarif aliwahi kutangaza kuwa  'Timu B' inayoundwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Bolton, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na Bin Zayed mrithi wa kiti cha ufalme wa Imarati (UAE) inajaribu kuisukuma Marekani kuanzisha vita vya kijeshi dhidi ya Iran.

 

Maoni