Sep 12, 2019 04:07 UTC
  • Rouhani: Ni lazima Marekani iachane na sera zake za vita na mashinikizo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, stratijia ya taifa la Iran katika kukabiliana na mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ni kusimama kidete. Ameongeza kuwa: "Ni lazima Marekani iweke kando sera zake za kupenda vita na mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa."

Rais Rouhani aliyasema hayo Jumatano mjini Tehran katika kikao cha baraza la mawaziri na kusisitiza kuwa, mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. Aidha amesema: "Katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Iran inategemea mantiki ya kutekeleza ahadi kwa sharti kuwa upande wa pili nao utekeleze ahadi na iwapo hautatekeleza ahadi zake katika JCPOA, Iran nayo pia haitatekeleza ahadi zake."

Rais wa Iran amebaini kuwa: "Hatua ya tatu ya kupunguza ahadi katika JCPOA ni hatua muhimu zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wala  haiwezi kulinganishwa na hatua mbili za awali na iwapo kutakuwa na udharura, basi katika siku za usoni Iran itachukua hatua zaidi katika kadhia hiyo."

Rais Rouhani amebaini kuwa, leo uso wa Jamhuri ya Kiislamu duniani unatambulika kama uso wa kutaka amani na misimamo ya wastani. Ameendelea kusema kuwa: "Iran haijawahi kuwa muanzishaji wa uvamizi na vikwazo wala haijakiuka majukumu na ahadi zake bali ni pande zingine ndizo ambazo zimekiuka ahadi zilizotoa."

Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 8 Mei 2019, mwaka mmoja baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA  na kushindwa nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao katika mapatano hayo, Iran imelazimika kuchukua hatua za kukabiliana na hali hiyo.

Katika fremu ya mapatano ya JCPOA, na kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya mapatano hayo, Iran ilianza kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika JCPOA na hadi sasa imechukua hatua tatu katika kadhia hiyo.

Hatua ya tatu ya Iran katika kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya JCPOA ilichukuliwa Septemba 6 2019, na katika fremu hiyo imeweka kando vizingiti kadhaa katika uga wa utafiti na ustawi wa miradi yake ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Tags

Maoni