Sep 17, 2019 08:13 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Hayatafanywa mazungumzo na Marekani katika ngazi yoyote ile

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kauli mpya zilizotolewa na Marekani kuhusu mazungumzo na akasisitiza kwamba: Viongozi wote wa Jamhuri ya Kiislamu wanakubaliana kwa kauli moja kuwa, hayatafanywa mazungumzo na Marekani katika ngazi yoyote ile.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo wakati wa ufunguzi wa darsa ya marhala ya juu kabisa ya Fiqhi sambamba na kuanza mwaka mpya wa masomo katika vyuo vikuu vya kidini hapa nchini vya Hawza.

Amesema, lengo la Marekani la kutumia mbinu ya mazungumzo ni kutaka kutwisha matakwa yake na kuthibitisha kuwa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa yamekuwa na taathira kwa Iran. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, sera za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa katika kukabiliana na taifa la Iran hazina maana wala thamani yoyote.

Ayatullah Khamenei ameashiria misimamo tofauti ya viongozi wa Marekani kuhusu mazungumzo na akasema: Baadhi ya wakati wanasema, ni mazungumzo bila masharti yoyote, na wakati mwingine wanasema, mazungumzo kwa kutekeleza kwanza masharti 12. Kauli kama hizi ama zinatokana na siasa zao za kuchanganyikiwa au ni mbinu ya kuukanganya upande wa pili. Lakini bila shaka Jamhuri ya Kiislamu haitababaika, kwa sababu njia tunayofuata iko wazi kabisa na tunajua tunachokifanya.

Ayatullah Khamenei akizungumza katika ufunguzi wa darsa ya fiqhi

Amesisitiza kuwa: Kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya aina hii inapasa wawaendee watu ambao, wanayowafanyia ni mithili ya ng'ombe wa kukamwa maziwa; lakini Jamhuri ya Kiislamu ni jamhuri ya waumini, jamhuri ya waliojisalimisha kwa Allah na jamhuri ya izza na heshima.

Kiongozi Muadhamu ameeleza bayana kwamba: Ikiwa Marekani itaachana na kauli zake hizo na kutubia, na ikarejea kwenye makubaliano ya nyuklia iliyoyakiuka, wakati huo ndipo nayo pia itaweza kushirki kwenye mazungumzo ya pamoja na nchi zingine shiriki kwenye makubaliano hayo, zinazofanya mazungumzo na Iran; kinyume na hivyo hakuna mazungumzo yatakayofanywa katika ngazi yoyote baina ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na Wamarekani, si New York, si pengine popote pale.../

 

Tags

Maoni