Sep 18, 2019 02:39 UTC
  • Kuonana Rouhani na Erdogan mjini Ankara; mazungumzo na makubaliano ya kupanua mabadilishano ya kibiashara kwa sarafu ya taifa hadi ushirikiano wa kiulinzi na kiusalama

Uhusiano wa Iran na Uturuki daima umekuwa wa kirafiiki na kidugu na serikali mbili na wananchi wa mataifa haya, wamekuwa pamoja na bega kwa bega katika mazingira tofauti.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu ya juzi alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki pambizoni mwa duru ya tano ya mkutano wa pande tatu wa Iran, Uturuki na Russia ambapo alibainisha juu ya kuanza hatua mpya ya uhusiano wa Tehran na Ankara.

Rais Rouhani sambamba na kusisitiza kwamba, kupanuliwa ushirikiano wa kibiashara wa Iran na Uturuki kwa kustafidi na sarafu za taifa katika mahusiano kunaleta harakati na kasi katika mahusiano ya kiuchumi ya pande mbili ameeleza kwamba, Iran inakaribisha kwa mikono miwili kuja hapa nchini wafanyabiashara wa Uturuki na kuwekeza katika sekta binafsi na hivyo kuendeshwa miradi ya pamoja baina ya pande mbili.

Naye Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki  ameashiria katika mazungumzo yake na Rais Rouhani juu ya uhusiano unaopanuka wa Iran na Uturuki na kueleza kwamba, vikwazo vya Marekani havijawa na taathira iliyokusudiwa na Washington. Kadhalika Rais wa Uturuki amesisitiza kuwa, Iran na Uturuki zimekuwa na zitaendelea kuwa pamoja na bega kwa bega katika kipindi kigumu.

Marais wa Iran, Uturuki na Russia walipokutana 16/09/2019 Ankara Uturuki

Ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi mbili hizo kwa kutumia sarafu za taifa umepiga hatua kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Abdul-Nasser Hemmati. Gavana Mkuu wa Benki Kuu ya Iran ametangaza kuwa, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na Uturuki kwa kutumia sarafu za taifa za nchi mbili hizo kwa sasa kimefikia asilimia 34. Inatarajiwa kuwa, kwa kufanyika kikao cha 27 cha Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Iran na Uturuki katika siku za usoni, kutaandaa fursa mpya kwa ajili ya pande mbili kustawisha zaidi ushirikiano wao katika nyuga mbalimbali.

Muhammad Perinçek mtaalamu wa Uturuki anaamini kuwa, Uturuki, Russia, Iran na Azerbaijan zinaweza kuanzisha muuungano wenye nguvu ambao utadhamini usalama wa eneo zima na  na kuleta msukumo wa ustawi.

Iran, Russia na Uturuki zilishirikiana na kuwa pamoja na serikali na wananchi wa Syria katika vita dhidi ya Daesh na ugaidi. Kwa mtazamo huo, ushirikiano wa nchi tatu hizo una umuhimu mkubwa. Ushirikiano huo hivi sasa pia umekuwa ukiendelea kwa kutumia uwezo na suhula zote. Katika uwanja huo, viongozi wa nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki wamekutana katika duru ya tano ya mazungumzo yao katika fremu ya mwenendo wa mazungumzo ya Astana na kueleza bayana kwamba, kuna udharura wa kuisaidia serikali ya Syria katika kupambana na mabaki ya magaidi hususan katika eneo la Idlib na mashariki mwa Furati na ushirikiano huu unapasa kuendelea hadi pale mizizi yote ya ugaidi itakapong'olewa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rais Rouhani na waziri wake wa mashauri ya kigeni wakiwa katika duru ya tano ya mkutano wa pande tatu wa Iran, Uturuki na Russia uliofanyika 16/09/2019 nchini Uturuki

Katika uwanja huo huo, Brigedia Jenerali, Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliongozana na Rais Hassan Rouhani katika safari yake nchini Uturuki ambapo katika mazungumzo yake na Hulusi Akar, Waziri wa Uloinzi wa Uturuki, wawili hao walibadilishana mawazo kuhusiana na masuala ya kiusalama na kiulinzi katika eneo.

Kwa hakika utambulisho wa mazungumzo ya Astana ni kufanya jitihada  za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria. Iran, Russia na Uturuki zimekuwa zikisisitiza juu ya kulindwa umoja wa ardhi ya Syria na kupinga vikali hatua zozote za kutaka kuigawa ardhi ya nchi hiyo.

Akitathmini matokeo ya ushirikiano huo, Rais Erdogan anasema: Ushirikiano wa pande tatu katika fremu ya mchakato wa mazungumzo ya Astana hadi sasa umekuwa na matokeo mazuri kwa ajili ya amani na uthabiti wa Syria na eneo kwa ujumla, na makubaliano ya nchi tatu yamezuia kutokea mauaji ya umati katika maeneo mbalimbali.

Mbali na matunda hayo, pia kumepigwa hatua ya kuzingatiwa kwa ajili ya kustawisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi baina ya nchi tatu hizo. Majimui ya mambo haya na mhimili wa mazungumzo ya marais wa Iran, Uturuki na Russia yanaonyesha kuwa, katika kiini cha ushirikiano huo wa pande tatu kuna uwanja na mazingira muhimu na ya kistratejia kwa minajili ya kupanua ushirikiano ambapo hilo lina mchango muhimu katika kuendelea mwenendo wa kusimama kidete mkabala na siasa za uingiliaji mambo za Marekani katika eneo hili la Mashariki ya Kati..

Maoni