Sep 18, 2019 03:17 UTC
  • Zarif: Njia pekee ya utatuzi ni kukomeshwa vita dhidi ya taifa la Yemen

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa wito wa kuhitimishwa vita nchini Yemen.

Katika jumbe zake mbili kwenye mtandao wa Twitter, Muhammad Javad Zarif ameashiria jinai za kivita zinazofanywa na wavamizi wa nchi ya Yemen wakisaidiwa na Marekani na kusema: Marekani inafanya makosa na iko njozini kama inadhani kwamba, wahanga wa jinai za kivita za miaka minne ya nusu huku Yemen hawatatumia nguvu zote walizonazo kwa ajili ya kujibu uhalifu na jinai hizo.

Zarif amesema kuwa, huenda Marekani inaona aibu kuona kwamba, silaha zake zilizonunuliwa na Saudi Arabia kwa mabilioni ya dola hazifui dafu mbele ya mashambulizi ya watu wa Yemen. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameashiria uzushi na uongo wa maafisa wa Marekani wanaodai kuwa, Iran imehusika katika mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya taasisi za mafuta huko Saudi Arabia na kusema: "Kutoa tuhuma dhidi ya Iran hakutabadilisha lolote; njia pekee ya utatuzi kwa pande zote ni kuhitimisha vita nchini Yemen."

Zarif amesema kuwa, Marekani kamwe haiumizwi na mauaji yanayofanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watoto wa Yemen lakini Wamarekani huumia tu pale Wayemeni wanaodhulumiwa wanapotoa jibu kwa jinai na uhalifu wa Saudia kwa kushambulia taasisi za mafuta za serikali ya Riyadh. 

Taasisi za mafuta za Saudia zikiteketea kwa moto

Jumamosi iliyopita kikosi cha ndege zisizo na rubani cha Yemen  kilirusha ndege 10 zilizotengezwa na Wayemen, na kushambulia vituo vya kusafishia mafuta vya Buqayq na Khurais, vya Shirika la Kitaifa la Mafuta la Saudia, ARAMCO na kusababisha hasara kubwa kwa Riyadh. Mashambulizi hayo yamesimamisha nusu ya uzalisha wa mafuta yote ya Saudi Arabia.  

Maoni