Sep 18, 2019 12:22 UTC
  • Iran yakanusha madai ya kuhusika na mashambulizi ya Aramco, Saudia, yaitahadharisha Marekani

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepinga tuhuma za wakuu wa Marekani kuwa eti Iran ilihusika katika mashambulizi yaliyolenga kituo kikubwa cha kusafisha mafuta cha Aramco nchini Saudi Arabia na kusisitiza kuwa: "Hakuna ushahidi, nyaraka wala dalili zilizowasilishwa na yote yanayosemwa ni madai tu."

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran na akifafanua zaidi kuhusu mashambulizi ya Wayemen dhidi ya kituo cha mafuta cha Aramco cha Saudia amesema: "Kumejiri mapigano baina ya Saudi Arabia na Yemen na Wayemen wamejibu jinai za Saudia."

Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka amani na usalama katika eneo. Ameongeza kuwa: "Iwapo Iran itakabiliwa na tishio basi itatoa jibu kali kama ilivyofanya wakati ilipotungua ndege isiyo na rubani ya Marekani.

Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa na kusema: "Madai ya wakuu wa Marekani kuwa eti Iran ilihusika na hujuma dhidi ya kituo cha Shirika la Mafuta la Aramco la Saudia ni uongo mtupu." Hayo yamo kwenye barua rasmi ambayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeuandikia Ubalozi wa Uswisi mjini Tehran (ambao unalinda maslahi ya Marekani nchini Iran).

Kituo cha Aramco kikiteketea moto Saudi Arabia baada ya kushambuliwa na ndege zisizo na rubani (drone) za Yemen

Taarifa hiyo imelaani madai ya Marekani kuwa eti Iran ilihusika katika kushambulia kituo cha mafuta ya Aramco na kusema: "Iran haikuhusika na mashambulizi hayo na madai ya Rais Donald Trump wa Marekani na Mike Pompeo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ni uongo mtupu."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeitahadharisha serikali ya Marekani kuwa, iwapo inalenga kutekeleza hujuma ya kijeshi dhidi ya Iran, basi hujuma hiyo itajibiwa haraka na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na upeo wa makabiliano hayo hautaishia katika chimbuko la tishio.

Kikosi cha droni cha jeshi na wapiganaji wa kujitolea wa Yemen Jumapili kilitangaza kuwa ndicho kilichohusika na shambulio dhidi ya vituo vya mafuta vya shirika la mafuta la Aramco katika viwanda vya kusafisha mafuta vya Abqaiq na Khurais vilivyoko mashariki ya Saudi Arabia. Msemaji wa Jeshi la Yemen, Jenerali Yahya Sare'a amesema oparesheni hiyo ni katika fremu ya haki ya kisheria ya watu wa Yemen kujibu jinai za muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen. Pamoja na hayo Marekani imekuwa ikidai kuwa Iran ndiyo iliyotekeleza mashambulizi hayo.

Maoni