Oct 20, 2019 03:02 UTC
  • Rais Rouhani: Taifa la Iran limesimama imara kukabiliana na Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa la Iran limesimama imara na kwa nguvu zote katika miaka mingi sasa kukabiliana na ubeberu wa Marekani na kwamba Marekani na mabeberu wenzake pamoja na vibaraka wao kamwe hawawezi kulipigisha magoti taifa hili la Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo usiku wa kuamkia leo wakati alipoonana na majeruhi wa kivita walioshiriki katika vita vya kujihami kutakatifu vya baina ya mwaka 1980 hadi 1988 vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran na kusema kuwa, majeruhi hao wa kivita walitoa mchango mkubwa katika kulilinda taifa la Iran na kuliletea ushindi wa kila upande.

Rais Rouhani amezungumzia pia mashinikizo na vikwazo vya kila upande vya maadui na kusisitiza kwa kusema: "Kwa bahati nzuri wananchi wa Iran wameweza kusimama imara mbele ya njama za maadui."

 

Amesema, serikali ya Marekani imejitoa bila sababu katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA na hivi sasa inalishinikiza kwa vikwazo taifa la Iran, lakini vikwazo vyake vitaendelea kufeli kutokana na muqawama wa taifa la Iran ya Kiislamu.

Vile vile amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel na viongzi wa Saudi Arabia na Marekani wako mstari wa mbele katika kulishinikiza taifa la Iran hivyo amesisitiza kuwa, hakuna njia nyingine isipokuwa kuendelea na muqawama na kusimama imara mbele ya njama hizo za kila namna za maadui.

Maoni