Oct 21, 2019 07:48 UTC
  • Iran inajitegemea kikamilifu katika sekta ya nyuklia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa inajitegemea kikamilifu katika shughuli zake za nyuklia na haipokei msaada wowote wa kigeni katika uga huo.

Hayo yamesemwa na Ali Asghar Zare'an msaidizi wa Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran ambaye ameongeza kuwa: "Asilimia 100 ya shughuli za sekta ya nyuklia za Iran zinategemea uwezo wa ndani ya nchi  na hivi sasa tumejitosheleza katika utengenezaji wa aina mbali mbali ya mashinepewa (centrifuge)."

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya mafanikio ya sekta ya nyuklia ya Iran mjini Kerman, Zare'an amesema Tanuri Nyuklia ya Maji Mazito ya Araq ambayo imekarabatiwa itakamilika katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Ameongeza kuwa, kuna wakati ambao nchi zingine hazikuwa tayari kuipa Iran hata mashinepewa moja lakini sasa maelefu ya mashinepewa zilizoundwa Iran zinaafanya kazi katika vituo vya nyuklia vya Fordow na Natanz.

Rais Rouhani akitembelea maonyesho ya mafanikio ya sekta ya nyuklia ya Iran

Ameongeza kuwa, suala muhimu zaidi ya mashinepewa ni uwezo wa Iran wa kuzalisha mada inayojulikana kama 'keki ya njano' ambayo ni malighafi ya kistratijia inayotumiwa katika sekta ya nyuklia. Amebaini kuwa, nchi zote zinaidhinishwa kununua keki ya njano lakini kuna wakati ambao Iran ilikuwa inazuiwa kununua mada hiyo ambayo sasa inajizalishia kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa shughuli zake za nyuklia zinafanyika kwa malengo ya amani ya kuzalisha nishati na pia katika sekta za tiba na kilimo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa fatuwa akitangaza kuwa silaha za nyuklia ni haramu.

Tags

Maoni