Oct 21, 2019 12:30 UTC
  • Sayyid Mousavi: Iran iko tayari kutekeleza hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kutekeleza hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari wa ndani na wa nje ambapo ameashiria matukio yanayohusiana na utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kueleza wazi kwamba, hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wa taifa hili katika JCPOA imeshaandaliwa na kwamba, Iran iko tayari kutekeleza hatua hiyo.

Abbas Mousavi amebainisha kwamba, nchi zilizobakia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zinapaswa kutekeleza ahadi na majukumu yao kwa mujibu wa makubaliano hayo ili ziifanye Iran isichukue uamuzi wa kutekeleza hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake katika makubaliano hayo.

Azimio nambari 2231 la Baraza la Usaama la Umoja wa Mataifa liliunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA 

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameashiria vurugu na maandamano ya Lebanon na kueleza kwamba, Tehran haiingilii masuala ya ndani ya mataifa mengine na ina matumaini kuwa, utulivu utarejea katika nchi hiyo kwa kuwa pamoja makundi na vyama vyote vya nchi hiyo.

Kuhusiana na juhudi za Uturuki za kutaka kuanzisha kambi ya kijeshi ndani ya ardhi ya Syria, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, serikali ya Uturuki inaweza kuanzisha kambi ya kijeshi katika maeneo yake ya mpakani, na siyo ndani ya ardhi ya Syria kwani kuanzisha kituo kama hicho ndani ya nchi hiyo ni jambo lisilokubalika na linahesabiwa kuwa ni kuvamia na kukiuka mamlaka ya nchi inayojitawala ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Tags

Maoni