Oct 22, 2019 11:50 UTC
  • Makeke ya Trump mbele ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Donald Trump Rais wa Marekani mwenye kubwabwaja sana tangu aingie ikulu ya White House amechukua mkondo wa sera za chuki na uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na utendaji wake umejikita katika mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Tehran ili kwa njia hiyo aweze kulifanya taifa hili lisalimu amri na kukubali matakwa ya Washington.

Kwa muktadha huo, kila baada ya muda fulani, Trump huibuka na kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya Iran.

Jumatatu ya jana tarehe 21 Oktoba Trump alitishia kwamba, ikilazimu ataishambulia kijeshi Iran. Rais huyo wa Marekani amesisitiza kuwa, endapo tutalazimika tutatoa pigo kwa Iran ambalo halijawahi kushuhidiwa hadi sasa na endapo kutakuwa na ulazima, basi tumejiandaa kwa ajili ya vita. Trump ameionya Tehran kwamba, Marekani ina jeshi lenye nguvu zaidi duniani, lakini pamoja na hayo, hadi sasa amekuwa akichukua hatua za kujizuia kwa hali ya juu kabisa.

Tukitupia jicho utendaji wa kiusalama wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi hususan katika Ukanda wa Ghuba ya Uajemi tunashuhudia bayana makeke na bwabwaja za Trump na jinsi vitisho vyake hivyo vilivyo tupu dhidi ya Iran. Licha ya kuungua meli za mafuta za washirika wa Washington katika eneo hili la Asia Magharibi, mashambulio dhidi ya taasisi za mafuta za Saudia za shirika la ARAMCO ambapo serikali ya Trump ilifanya njama za kunasibisha hilo la Iran na hata kutunguliwa na Iran droni ghali ya Global Hawk ya  Washington lakini serikali ya Trump pamoja na kutoa vitisho vingi, haijathubutu kutekeleza hatua yoyote ile ya kijeshi dhidi ya taifa hili.

Donald Trump akitia saini vikwazo dhidi ya Iran

Baada ya ndege ya Marekani isiyo ya rubani kutunguliwa, Trump alidai kwamba, ana mpango wa kulipiza kisasi dhidi ya hatua hiyo ya Iran, lakini kutokana na kuzingatia masuala ya kibinadamu alitupilia mbali mpango wake huo. Pamoja na hayo, kimsingi yalikuwa ni makeke na madai matupu. Hapana shaka kuwa, hofu na woga wa Marekani wa kukabiliana kijeshi na Iran unatokana na uwezo mkubwa wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu, ushawishi mkubwa wa taifa hili katika eneo na kuwezekana kupata kipigo kikubwa vikosi vya Marekani vilivyoko katika eneo mkabala na mashambulio ya ulipizaji kisasi ya Iran.

Trump ambaye kwa sasa amekumbwa na utendaji unaokinzana na kugongana katika sera zake za kigeni na hali ya kutoaminiwa Marekani inayoongezeka kila leo hata baina na washirika wa Washington,  anafanya juhudi za kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya Iran ili sambamba na kutunisha misuli awaliwaze washirika wake katika eneo la Asia Magharibi kwamba, Washington inawaunga mkono.

Lengo la serikali ya Marekani ni kuleta umoja wa kimataifa utakaokuwa dhidi ya Iran, kuandaa mazingira na visingizo vya kutekeleza mashinikizo ya kiuchumi, kushadidisha hatua kali dhidi ya Tehran, kuandaa uwanja wa kuongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo mla Ghuba ya Uajemi na kuleta anga ya kuaminiwa baina ya washirika wake katika eneo.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Filihali Marekani imo mbioni kuanzisha muungano wa baharini kwa ajili ya kile kinachodaiwa kuwa, kudhamini usalama na uhuru wa meli katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz.

Pamoja na hayo, uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani katika eneo hili wenye lengo la kudhamini amani na usalama wa washirika wake, haujawa na faida wala matunda yoyote yale. Tab'an, Trump ametangaza kuwa, kudhaminiwa usalama huo kwa washirika wake kuna gharama zake. Akizungumza Jumatatu ya jana katika mahojiano na Kanali ya Televisheni ya Fox News Donald Trump alitangaza kuwa, Saudi Arabia imekuwa ikinunua na kulipia gharama ulinzi na himaya ya Marekani kwake na hivi sasa gharama inazotoa Riyadh kwa ajili ya hilo haijawahi kushuhudiwa.

Pamoja na yote hayo, lakini matamshi mapya ya Trump yamezusha maswali mengi kuhusiana na kubadilika nadharia ya kijeshi ya Marekani katika Ghuba ya Uajemi. Kwa upande mmoja Trump daima amekuwa akisisitiza juu ya kuondoa vikosi vya nchi yake katika eneo na kwa upande wa pili amekuwa akitoa vitisho vya kuishambulia kijeshi Iran.

Tags

Maoni