Oct 22, 2019 14:49 UTC
  • Iran yaitaka UN kushiriki katika uchunguzi wa shambulizi dhidi ya meli ya mafuta ya SABITI

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameutaka umoja huo ushiriki katika uchunguzi kuhusu shambulizi lililolenga meli ya mafuta ya Iran inayojulikana kwa jina la SABITI.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa Tehran imeanza uchunguzi wake kuhusiana na shambulizi dhidi ya meli ya mafuta ya Iran ya SABITI na imemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kutuma wataalamu wa umoja huo kwa ajili ya kushiriki katika uchunguzi huo. 

Taarifa hiyo imesema shambulizi lililolenga meli ya SABITI lilifanyika kwa ushiriki wa vibaraka wa nchi fulani na ni hujuma ya kigaidi. 

Meli ya mafuta ya SABITI ilishambuliwa mara mbili Ijumaa ya tarehe 11 mwezi huu wa Oktoba wakati ilipokuwa katika njia ya majini mashariki mwa Bahari Nyekundu. Mashambulizi hayo mawili dhidi ya meli ya mafuta ya SABITI yalipishana kwa takriban nusu saa. Meli hiyo iliingia katika maji ya Iran Jumatatu ya jana. 

Katika miezi kadhaa iliyopita kumefanyika vitendo vya uharibifu dhidi ya meli za mafuta za Iran katika Bahari Nyekundu na uchunguzi unaendelea kufanywa ili kubaini ni nani wanaohusika na chokochoko hizo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia, shambulizi dhidi ya meli ya mafuta ya Iran inayojulikana kama SABITI lilitekelezwa na serikali moja au serikali kadhaa.  

Meli hiyo ilishambuliwa ikiwa umbali wa maili 60 kutoka bandari ya Jeddah ya Saudi Arabia.  

Maoni