Nov 13, 2019 11:54 UTC
  • Rouhani: Taifa la Iran limevunja njama za Marekani kwa mapambano

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria njama za Marekani za kutoa pigo kwa taifa la Iran na kusema: "Mapambano (muqawama) ya wananchi wa Iran yamevunja njama za Marekani."

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran wakati alipohutubu katika kikao cha waandishi habari na kuongeza kuwa: "Watu wa Iran kwa kusimama kidete na kwa muqawama, wameweza kuvunja njama za adui." Amesisitiza kuwa Iran katu haitasalimu amri."

Rais Rouhani aidha ametuma salamu za kheri na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad Al Mustafa SAW na pia  kwa mnasaba wa Maulid ya Imam Jaafar Sadiq AS, Imam wa Sita wa Mashia na kuongeza kuwa: "Katika wikii ya Umoja wa Kiislamu, kama ambavyo Mtume wa Uislamu SAW anapaswa kuwa kigezo cha umoja kwa Waislamu wote, Imam wa Sita wa Mashia pia naye anapaswa kuwa kigezo cha umoja kwa Waislamu."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Imam Sadiq AS , alikuwa Imamu mwenye kuweka mambo wazi na kubainisha uhakika kwa Mashia na Masunni katika ulimwengu wa Kiislamu na pia kwa harakati kubwa ya kielimu duniani. Ameongeza kuwa: "Katika mafunzo ya Imam Sadiq AS kulikuwa na masomo ya sayansi ya kemia, fizikia, biolojia na falsafa."

Umoja wa Waislamu

Tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka 1441 Hijria Qamaria inayosadifiana na 15 Novemba 2019 ni Maulid au siku ya kukumbuka uzawa wa Mtume Muhammad SAW na Imam Jaafar Sadiq AS.

Kuhusu chimbuko la Wiki ya Umoja wa Kiislamu inafaa kuashiria hapa kuwa, Ahlu Suna wal Jamaa wanategemea baadhi ya riwaya katika kuamini kwamba Mtume Mtukufu SAW alizaliwa tarehe 12 Rabiul Awwal nao Waislamu wa madhehebu ya Shia wana riwaya nyingine nyingi zinazowafanya waamini kuwa Mtume SAW alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal. Kipindi cha kati ya tarehe hizo mbili kilitangazwa na Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ili kuleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu bila kujali madhehebu zao.

Tags

Maoni