Nov 14, 2019 02:43 UTC
  • UN yaitaka US iiondolee Iran vikwazo kama ilivyoagizwa na ICJ

Umoja wa Mataifa umeitaka Marekani iheshimu agizo la Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu la kuiondolea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vinavyohusiana na bidhaa za kibinadamu.

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq ambaye alisisitiza kuwa, "Tunaziomba nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zifute vikwazo vyao dhidi ya Iran kwa mujibu wa uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu."

Afisa huyo wa UN alisema hayo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari wa shirika la habari la IRNA, aliyemuuliza juu ya msimamo wa umoja huo kuhusu vifo vya watoto kadhaa wa Kiirani waliokuwa wanaugua ugonjwa hatari wa ngozi wa Epidermolysis bullosa EB, kwa kukosa dawa na matibabu kutokana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya taifa hili.

Wakati huohuo, Hujjatul Islam Sayyid Hamid Reza Hashemi Golayegani, Mkuu wa Asasi Isiyo ya Kiserikali (NGO) inayowasaidia wagonjwa wa EB ameikosoa vikali Marekani kwa kushadidisha vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya taifa hili, ambavyo vimefanya kuwa vigumu kuingiza humu nchini dawa za kutibu watu wanaogua ugonjwa huo. 

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ)

Inakadiriwa kuwa kuna wagonjwa 1,200 wa Epidermolysis Bullosa  EB hapa nchini. Ugonjwa huu wa kurithi hufanya ngozi kuwa dhaifu na kuwa na uvimbe wenye maji maji.

Mwezi Machi mwaka huu, ICJ iliiagiza serikali ya Marekani kwamba hadi ifikapo tarehe 16 Mei mwaka huu, iwe imeshaeleza ni hatua gani imechukua kwa ajili ya kutekeleza amri ya mahakama hiyo ya kimataifa iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi, kuhusiana na kuondoa vikwazo vya dawa, chakula, vipuri vya ndege na huduma za anga dhidi ya Iran.

 

Tags

Maoni