Nov 15, 2019 01:23 UTC
  • Iran, muungaji mkono halisi wa Wapalestina katika kukabiliana na Israel

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko mstari wa mbele katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani katika kuwatetea watu wa Palestina.

Hassan Rouhani aliyasema hayo Alhamisi asubuhi mjini Tehran wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu na kuongeza kuwa, Palestina na Quds Tukufu ni maudhui mbili muhimu zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu hivi leo. Rais Rouhani ameashiria sera za Marekani na utawala wa Kizayuni za kutaka kadhia ya Palestina isahaulike na kusema: "Ulimwengu wa Kiislamu hautawaruhusu maadui  kusahaulisha kadhia ya Palestina ambayo ni kadhia ya kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu."

Kadhia ya ukombozi wa Palestina na Quds Tukufu (Jerusalem), kama maudhui muhimu zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu, daima imekuwa ikizingatiwa na kupewa kipaumbele katika mikutano ya kimataifa ya Umoja wa Kiislamu ambayo hufanyika mjini Tehran kila mwaka na nukta hiyo inaashiria umuhimu wa kuunga mkono taifa madhulumu la Palestina katika sera za kigeni za Iran.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, kuunga mkono ukombozi wa Palestina na Quds Tukufu ni mambo ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele cha kwanza katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kutangazwa Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa 'Siku ya Quds' ni ishara ya umuhimu wa kadhia ya Palestina katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, Tehran

Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiye aliyetangaza Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa 'Siku ya Quds' ili kwa njia hiyo kubakisha hai kadhia ya ukombozi wa Palestina duniani.

Hatua hiyo ya Imam Khomeini MA, mbali na kuhuisha fikra za mataifa ya Kiislamu na mataifa mengine yanayopigania uhuru duniani kuzingatia kibla cha kwanza cha  Waislamu, pia ilipelekea kusambaratika njama za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Palestina na Quds Tukufu.

Leo, kuliko wakati mwingine wowote ule, kuna haja kwa mataifa ya Kiislamu kuwa macho kwani Wazayuni wanaopata uungaji mkono wa Marekani na pia baadhi ya tawala za Kiarabu wanataka kadhia ya Palestina isahaulike.

Kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu, mpango wa eti 'Muamala wa Karne' wenye lengo la kuwapokonya kikamilifu Wapalestina ardhi zao na uhusiano wa siri wa baadhi ya tawala za Kiarbau na Israel ni mambo ambayo yanafanyika kwa lengo moja tu nalo ni kuunda makao salama kwa utawala wa Kizayuni unaolegalega na wakati huo huo kufanya kadhia ya Palestina isahahulike.

Wazayuni ni adui wa pamoja wa mataifa ya eneo na nchi zote za Kiislamu na katika kipindi cha miaka 70 iliyopita. Hata hivyo kutokana na hatua ya baadhi ya tawala za Kiarabu kutaka kuwa na uhusiano na utawala huo bandia ambao pia  unapata uungaji mkono wa Marekani, kuna njama ya kupotosha fikra za umma kuhusu adui wa pamoja wa mataifa ya Kiislamu na kwa msingi huo maadui wanatekeleza sera za chuki dhidi ya Iran au Iranophobia katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Katika hali kama hiyo na kwa kuzingatia kuwa, katika miongo mitatu iliyopita Marekani na utawala wa Kizayuni zimekuwa chimbuko la kila vita, mauaji na migongano baina ya mataifa y Asia Magharibi, kupatikana umoja wa mataifa ya Kiislamu na kuwa macho mataifa hayo mbele ya njama za Wazayuni ni jambo la dharura.

Mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel

Kama alivyosema, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika Kongamano la 33 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran, "Kizazi cha vijana kinapaswa kutambua kuwa, Marekani haijawahi kuwa na wala haitakuwa rafiki wa mataifa ya eneo na Waislamu na utatuzi wa matatizo ya eneo unapaswa kuwa mikononi mwa wananchi na Palestina inapaswa kukombolewa na Wapalestina na Waislamu shujaa katika eneo."

Kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni katika ardhi za Palestina kuanzia 'Quds hadi Ghaza', Waislamu kote duniani wanapaswa kuwa macho na uungaji mkono wao kwa Wapalestina wanaodhulumiwa ni nukta ambayo itazima njama zote za Wazayuni.

Kuhusiana na nukta hii, Ayatullah Mushin Araki, katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema, kuunga mkono muqawama na mapambano ya Wapalestina ni wajibu wa wote na kuongeza kuwa: "Umoja wa Kiislamu utavunja njama za mustakbirina dhidi ya Palestina."

Tags

Maoni