Nov 17, 2019 12:09 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Maadui wa Iran muda wote wanafikiria kuharibu usalama wa Iran tu + Video

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba wanachofikiria maadui siku zote ni kuharibu usalama na utulivu wa taifa la Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo asubuhi kwenye darsa ya juu kabisa ya fiqh na huku akiashiria mpango wa kudhibiti matumizi ya mafuta nchini Iran amesema kuwa, wataalamu wametofautiana kuhusu njia za kulifanikisha suala hilo lakini tangu huko nyuma nilisema kuwa, kama mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) itachukua uamuzi, basi mimi nitauunga mkono.

Ameongeza kuwa, mihimili hiyo mitatu imechukua maamuzi yao kwa kutegemea uchunguzi wa wataalamu hivyo inabidi maamuzi hayo yatekelezwe. Ni wazi kwamba baadhi ya wananchi wameingiwa na wasiwasi na hofu kuhusu uamuzi huo  au pengine yanaweza kuwa ni kwa madhara yao, lakini kufanya uharibifu na kuchoma moto maeneo ya umma si kazi ya wananchi, bali ni ya watu waovu.

 

Vile vile amesisitiza kuwa, maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na wa taifa la Iran muda wote wanaunga mkono uharibifu kama huo na kuongeza kuwa, mtu yeyote mwenye akili timamu na anayeipenda nchi yake, hawezi kufanya vitu kama hivyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, matukio kama hayo yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa kila nchi na jamii, na kuongeza kuwa, viongozi wote humu nchini wanapaswa kuwa macho kikamilifu na kuhakikisha kuwa mpango huo hauwasababishii matatizo. 

Itakumbukwa kuwa, siku ya Ijumaa, serikali ya Iran iliamua kukata ruzuku ya mafuta iliyokuwa ikiitoa ingawa hata hivyo, bado bei ya mafuta nchini Iran ndiyo ya chini zaidi duniani. Jambo hilo limetumiwa vibaya na maadui wa Iran kujaribu kuchochea machafuko humu nchini. 

Maoni