Nov 21, 2019 09:47 UTC
  • Udharura wa kustawishwa uhusiano wa kijeshi na kiusalama wa Iran na Pakistan, mbali na uhusiano wa kisiasa na kiuchumi

Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Pakistan ambaye amekuja nchini Iran akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kijeshi wa nchi yake, ameonana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, Mkuu wa Majeshi ya Iran, Kamanda Mkuu wa Jeshi na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika mazungumzo yake na Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Pakistan hapa Tehran, Rais Hassan Rouhani alisema: Tayari Iran imeshalifikisha kwenye mipaka ya Pakistan bomba la gesi maarufu kwa jina la bomba la amani, na kwamba Tehran iko tayari kushirikiana kikamilifu na Islamabad katika nyuga zote.

Vile vile amegusia matukio muhimu ya eneo la Asia Magharibi na kusema: Iran inaamini kwamba masuala na uhusiano wa kieneo wa nchi zote unapaswa kuwekwa kwa kuzingatia kuimarisha amani, utulivu na uthabiti kwenye eneo hilo.

Siku ya Jumatatu pia Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran alionana na Qamar Javed Bajwa, Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Pakistan na pande mbili zilijadiliana masuala ya kiulinzi, kijeshi na kiusalama yanayozihusu nchi hizo mbili jirani.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran (kulia) katika picha ya pamoja na Qamar Javed Bajwa, Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Pakistan

 

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wa ngazi za juu wa kijeshi wa Iran na Pakistan walisisitizia umuhimu wa kuwepo ushirikiano wa nchi zao katika masuala ya kiulinzi, kijeshi na kiusalama na kusema kuwa hilo ni jambo la dharura kama ulivyo udharura wa kuimarishwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hizi mbili. Kwenye mazungumzo hayo, Meja Jenerali Baqeri alitilia mkazo wajibu wa kuimarishwa ushirikiano katika kulinda utulivu na amani ya kudumu, usalama mipakani, kuzuia magenge ya kigaidi kuingia na kutoka kwenye mipaka hiyo, kupambana na magendo, kuwa na mipaka yenye harakati nyingi za kiuchumi, kusahilisha miamala ya kwenye mipaka na kuwa na misimamo inayofanana katika masuala ya ulimwenu wa Kiislamu.

Ukweli ni kwamba eneo la Asia Magharibi hivi sasa linapitia kipindi kigumu sana na kuna njama hatari zinafanyika dhidi ya nchi za eneo hili, hivyo kuna haja ya kuweko mashauriano kati ya nchi zote, na bila shaka ziara ya Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Pakistan hapa Tehran imefanyika kwa lengo hilo hilo.

Nchi mbili za Kiislamu za Iran na Pakistan zina mpaka mkubwa wa nchi kavu

 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, Iran inapaswa kuendelea kutumia uwezo wake wote kustawisha na kupanua mawasiliano na nchi mbalimbali duniani hususan majirani zake kadiri inavyowezekana. Jambo hilo linaweza kufanyika kwa njia mbalimbali ikiwemo ya udiplomasia wa kiuchumi, udiplomasia wa kisiasa n.k, katika kona zote za dunia.

Wachambuzi hao wa mambo wanasema pia kuwa, changamoto za kiusalama za eneo hilo, msababishaji wake mkuu ni Marekani inayoingilia kibeberu masuala ya ndani ya eneo hili. Maafa yanayofanyika leo kwenye eneo la Asia Magharibi kama vile kushambuliwa kinyama na kikatili wanawake na watoto wadogo wasio na hatia huko Yemen, kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina pamoja na mipango wa Kimarekani - Kizayuni inayotolewa mara kwa mara kama ule uliopachikwa jina la "Muamala wa Karne" ambao lengo lake hasa lilikuwa ni kuyaangamiza kikamilifu malengo matukufu ya taifa la Palestina, ni miongoni mwa masuala ambayo inabidi yakomeshwe kwa njia yoyote ile na hilo halitowezekana bila ya kuwepo ushirikiano wa kweli wa nchi za eneo hili.

Iran inasema kuwa, nchi jirani ndizo zinazojua uchungu wa eneo lao na ndizo zinazopaswa kujitatulia wenyewe masuala yao bila ya uingiliaji wa madola ajinabi

 

Kwa hakika kuanza kutembeleana maafisa wa kijeshi wa Iran na Pakistan ni sawa na kufunguliwa ukurasa mpya wa uhusiano wa nchi hizi mbili ndugu za Kiislamu. Ziara hizo zinaweza kuhesabiwa kuwa ni hatua muhimu sana katika uhusiano wa kiistratijia wa nchi hizo. Katika kipindi cha miaka kadhaa sasa, viongozi wa ngazi za juu wa kijeshi wa nchi hizi mbili wamekuwa wakitembeleana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala tofauti na ziara hizo zimekuwa zikitoa ujumbe wa kila namna wa kiusalama unaozihusu nchi mbili na wenye manufaa makubwa kieneo na kimataifa. Inaonekana ni kwa sababu hiyo pia ndio maana viongozi wengine wa Iran na Pakistan nao wakawa wanasisitiza kwamba kuna udharura wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa kijeshi na kiusalama baina ya Tehran na Islamabad sambamba na ule wa kisiasa na kiuchumi.

Maoni