Dec 03, 2019 12:08 UTC
  • Mkurugenzi Mkuu mpya wa wakala wa IAEA na mustakabali wa JCPOA

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ukiwa asasi ya usimamizi ya Umoja wa Mataifa kwa taasisi na shughuli za nyuklia za nchi wanachama, una nafasi muhimu mno katika kudhamini shughuli za nyuklia za wanachama wake na vilevile kueneza matumizi ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) jana Disemba Pili aliidhinishwa rasmi kuchukua wadhifa huo katika mkutano mkuu wa wakala huo uliofanyika mjini Vienna Austria. Akizungumza mbele ya waandishi wa habari baada ya kuchukua rasmi usukani huo alisema kuwa, ana matarajio makubwa kwamba taasisi hiyo itakuwa na uhusiano chanya na amilifu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba, anakaribisha hilo kwa mikono miwili.

Grossi ameongeza kusema kuwa, baadhi wanasema ni lazima kuwa na misimamo thabiti na ya kiadilifu mkabala na Iran, lakini mimi ninasema kuwa, tunapaswa kuwa na misimamo imara na kufanya mambo kwa insafu kwa wote. Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesisitiza kuwa, ukaguzi wa IAEA katika kipindi cha uongozi wake utafanyika kwa uadilifu sio tu kwa Iran bali kwa nchi zote wanachama. Rafael Grossi ambaye ni raia wa Argentina amesema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakusudia kubainisha mitazamo na matarajio yake kuhusiana na mwenendo wa uchukuaji hatua wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ambapo binafsi ninalipokea na kulikaribisha jambo hilo kwa mikono miwili.

Makubaliano ya nyuklia ya Mapngo Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA)

Kuchaguliwa Grossi kushika wadhifa huo hasa katika kipindi hiki nyeti cha makubaliano ya nyuklia  ya JCPOA kumekuwa na umuhimu maradufu. Troika ya Ulaya inayojumuisha nchi za Ufaransa, Ujerumani, Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya baada ya kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA Mei, mwaka 2018, iliahidi kwamba, itadhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran na hivyo kuyalinda na kuyabakisha makubaliano hayo muhimu kwa ajili ya amani na uthabiti wa kimataifa.

Licha ya madola ya Ulaya kukosoa utendaji wa Marekani ulio dhidi ya JCPOA na hata kutoa ahadi chungu nzima kwa Iran kuhusiana na kutekeleza mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha na Iran kwa jina la INSTEX, lakini mpaka sasa hazijachukua hatua yoyote ile ya maana kwa ajili ya kutekeleza ahadi na majukumu yao.

Katika kukabiliana na hatua hizo za kulegalega za madola ya Ulaya, Mei 8 mwaka huu iliyosadifiana na kutimia mwaka mmoja tangu Marekani ijitoe katika makubaliano hayo, Iran ilianza kupunguza hatua kwa hatua uwajibikaji wake katika makubaliano hayo ya nyuklia ambapo hadi sasa imeshakuchua hatua nne.

Kwa kuzingatia kuchaguliwa na kuidhinishwa rasmi Rafael Grossi kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa IAEA, taasisi ambayo ina jukumu la kusimamia shughuli za nyuklia za mataifa ya dunia, inaonekana kuwa, moja ya majukumu yake muhimu kabisa ni makubaliano ya nyuklia pamoja na mustakabali wa makubaliano hayo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara nyingi juu ya ulazima wa kuweko utendaji wa kiadilifu na usiopendelea upande wowote wa wakala wa IAEA katika uga wa shughuli za nyuklia za nchi wanachama ikiwemo Iran. Akizungumza hapo jana Jumatatu, Grossi aliahidi kuwa atakuwa muadilifu kwa nchi zote wanachama. Kwa muktadha huo inatarajiwa kuwa, hataathirika na mashinikizo na ushawishi hususan wa Marekani na atafanya shughuli zake kwa uadilifu kuhusiana na hatua za Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Kwa kuzingatia kwamba, kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 Rafael Grossi alikuwa Naibu wa Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa zamani IAEA katika masuala ya siasa na alikuwa na misimamo mikali kuhusiana na Iran, Tehran ilikuwa na wasiwasi kuhusiana na kuchaguliwa mwanadiplomasia huyo kushika wadhifa huo.

Kazem Gharib Abadi, Balozi na Mwakilishi wa Iran katika wakala wa IAEA

Akizungumzia kuchaguliwa mkurugenzi mkuu huyo mpya, Kazem Gharib Abadi, Balozi na Mwakilishi wa Iran katika wakala wa IAEA amesema kuwa, Tehran inatumai kwamba, uhusiano wake na taasisi hiyo utakuwa chanya, na wakala huo utaendesha shughuli zake kwa njia huru na bila kuegemea upande wowote.

Msimamo wa Iran mkabala na Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) mbali na kubainisha wasiwasi na daghadagha, unasisitiza juu ya kutopendelea upande wowote na kufanya mambo kwa uhuru kamili bila ya kuathiriwa na mashinikizo kuhusiana na miradi ya nyuklia ya Tehran yenye malengo ya amani hususan makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, hasa kwa kutilia maanani kwamba, hatua zote za Iran ziko wazi na zinafanyika katika mkondo wa JCPOA.

Ukweli wa mambo ni kuwa, utendaji huu wa Iran haujaacha mwanya wa visingizio. Ukweli huu umeungwa mkono na ripoti 16 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambapo zimeeleza bayana kwamba, Iran imefungamana na kutekeleza kikamilifu majukumu yake.

Tags

Maoni