Dec 06, 2019 10:30 UTC
  • Sergei Ryabkov
    Sergei Ryabkov

Baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei mwaka 2018 wanachama wengine wa makubaliano hayo wamekuwa wakitilia mkazo udharura wa kulindwa mapatano hayo ya kimataifa kutokana na umuhimu wake katika kulinda amani na usalama wa kimataifa.

Pamoja na hayo nchi za Ulaya wanachama katika makubaliano hayo zimezembea sana katika kutekeleza vipengee vyake. Suala hilo ndilo lililoifanya Russia, kama mwanachma wa kundi la 4+1, kutahadharisha juu ya uwezekano wa kusambaratika makubaliano hayo. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov Alkhamisi ya wiki hii alitahadharisha kwamba, matatizo yanayohusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanazidi kurundikana, sauala ambalo yumkini likatatiza jitihada za kuokoa makubaliano hayo. Ryabkov amesema kuwa: "Matatizo ambayo hayajatatuliwa yanazidi kurundikana; hivyo yumkini tukajikuta katika hali mbaya zaidi kutokana na mienendo ya wanachama wa JCPOA ya kushindwa kulindwa mapatano hayo, na hatua za Iran za kupunguza utekelezaji wa baadhi ya vipengele vyake." Ryabkov leo Ijumaa alitarajiwa kushiriki kikao cha kamisheni ya makatibu wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje wa Iran na nchi wanachama katika kundi la 4+1. Kikao cha leo kinafanyika mwezi mmoja baada ya Iran kuchukua hatua ya nne ya kupunguza utekeleza wa baadhi ya vipengee vya makubaliano ya JCPOA baada ya nchi za Ulaya kushindwa kudhamini maslahi yake ndani ya makubaliano hayo. 

Sergei Ryabkov

Ryabkov pia ameikosoa troika ya Ulaya kutokana na kusalimu amri mbele ya njama zinazofanywa na Marekani kwa ajili ya kuharibu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Russia ametahadharisha kuwa, yumkini nchi za Ulaya zikajikutaka katika hali ya kukubali kutwisha matakwa ya kisiasa ya Marekani. Amesema: "Kwa hali yoyote ile suala la kusambaratika mapatano ya JCPOA ni jambo baya sana; kwanza kutokana na matokeo yake mabaya katika mfumo wa kuzuia silaha za maangamizi, na pili katika upande wa kukiuka haki ya kujitawala ya nchi mbalimbali."

Baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei mwaka 2018, Umoja wa Ulaya hususan troika ya umoja huo inayojumuisha nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, uliahidi kwamba, utalinda maslahi ya Iran katika mapatano hayo kupitia taratibu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha uliopewa jina la INSTEX. Pamoja na hayo hadi sasa nchi hizo hazijachukua hatua ya maana katika uwanja huo licha ya kupinga kwa kauli tu hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mapatano hayo. 

Mwaka mmoja baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa na kuthibitika kwamba, mapendekezo ya Ulaya ya kufidia hasara za kiuchumi za Iran zilizosababishwa na kujiondoa Marekani hayafui dafu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikomesha subira yake ya kistratijia na kutangaza kwamba, inasitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo kwa kutegemea vifungu nambari 26 na 36 vya JCPOA. Hata hivyo imesisitiza kuwa itatekeleza tena vipengee hivyo mara baada ya washirika wengine katika makubaliano hayo kutekeleza majumuku yao. Katika uwanja huo, naibu balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Eshagh Al Habib anasema: "Iran haiwezi tena, haipaswi na haitaki kuendelea kubeba peke yake mzigo wa makubaliano ya JCPOA."

Eshagh Al Habib

Jambo la kushangaza ni kwamba, badala ya kufidia makosa yao katika utekelezaji wa makubaliano hayo ya nyuklia, nchi za Ulaya zimetoa taarifa ya vitisho dhidi ya Iran. Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa: "Katika kikao cha leo, nchi za Ulaya zitaitaka Iran ikomeshe "ukiukaji" wa vipengee vya makubaliano ya JCPOA la sivyo yumkini vikwazo vya Umoja wa Mataifa vikaanza kutekelezwa tena dhidi ya nchi hiyo." 

Hata hivyo Tehran inaendelea kusisitiza kuwa, suala la kuitaka Iran itekeleze peke yake vipengee vyote vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA huku wanachama wengine wa makubaliano hayo wakiendelea kuyapuuza halikubaliki, ni kinyume cha sheria na mantiki na linapingana na maslahi yake ya kitaifa. Hivyo, badala ya kutoa vitisho vya kulipeleka tena faili la JCPOA katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutishia kuiwekea vikwazo Iran, nchi za Ulaya zinapaswa kurekebisha mienendo yao kuhusiana na makubaliano hayo na kutekeleza majumu yao kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano hayo; wakati huo ndipo Iran itakapotekeleza tena majukumu na hadi zake zote. 

Tags

Maoni