Dec 08, 2019 04:55 UTC
  • Zarif: Mafanikio ya kisayansi ya wasomi Wairani ni mwiba katika macho ya maadui

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, Marekani imekuwa ikijaribu kuzuia ustawi wa Iran lakini haijaweza kufanikiwa.

Zarif ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad katika sherehe ya kumpokea Dakta Masoud Suleimani, mwanasayansi Muirani ambaye amerejea nchini baada ya kushikiliwa kinyume cha sheria nchini Marekani kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Zarif ameongeza kuwa, Dkt  Suleimani alishikiliwa mateka na Marekani kwa muda wa miezi 14 bila sababu yoyote na kuongeza kuwa: "Mafanikio ya kisayansi ya wasomi Wairani ni mwiba katika macho ya maadui wa taifa la Iran." Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Dakta Suleimani alipewa mapendekezo mara kadhaa kuwa asirejee Iran bali abaki Marekani lakini mwanasayansi huyo mzalendo alikataa vishawishi hivyo vya Wamarekani.

Dkt Masoud Suleimani amewaambia wanaandishi habari kuwa, lengo la Marekani katika kumshikilia mateka ni kuendeleza uhasama na taifa la Iran. Ameongeza kuwa, wakuu wa Marekani walimetenganisha na wafungwa wengine gerezani na kudai kuwa yeye ni gaidi lakini hawakuweza kuthibitisha madai hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Javad Zarif (kulia) akizungumza na waandishi habari akiwa ameandamana na Dakta Masoud Suleimani katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad, Tehran 07 Disemba 2019

Baada ya kushikiliwa kwa muda wa miezi 14 kinyume cha sheria nchini Marekani, hatimaye jana mjini Geneva Uswisi, Dakt Masoud Suleimani aliachiliwa huru na kukabidhiwa wakuu wa Iran na baada ya hapo akapanda ndege kurejea Iran akiwa ameandamana na Mohammad Javad Zarif.

Dkt. Suleimani ameachiliwa huru baada ya ufuatiliaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa ushirikiano na vyombo vya usalama na mahakama nchini pamoja na  ushirikiano wa serikali ya Uswisi.

Katika mchakato huo ambao uliidhinishwa na Baraza la Usalama wa Taifa Iran, Xiyue Wang, raia wa Marekani mzaliwa wa China, ambaye alikuwa anahudumia kifungo cha miaka 10 gerezani nchini Iran baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi, ameachiliwa huru katika hatua ya huruma ya Kiislamu. Jasusi huyo amekabidhiwa wakuu wa Uswisi na amerejea Marekani.

Ikumbukwe kuwa mnamo Oktoba 25, 2018, Profesa Suleimani ambaye ni mwanasayansi wa seli shina na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Tarbiat Modares, alifika katika uwanja wa ndege wa Chicago kufuatia mwaliko wa taasisi moja ya utafiti Marekani ya Mayo. Punde baada ya kuwasili, Profesa Suleimani alitiwa mbaroni na makachero wa FBI na tokea wakati huo alikuwa katika kizuizi bila kuruhusiwa kuwa na mawasiliano yoyote na jamaa zake.

Tags

Maoni