Dec 08, 2019 07:34 UTC
  • Rais Rouhani awasilisha bungeni bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 1399 Hijria Shamsia

Rais Hassan Rouhani amewasilisha bungeni bajeti ya serikali ya mwaka ujao wa fedha wa 1399 Hijria Shamsia.

Akiwasilisha bajeti hiyo ya mwaka ujao wa fedha hii leo mbele ya wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, bajeti ya mwaka ujao ni bajeti ya istiqama na ya kukabiliana na vikwazo; na akasisitiza kwamba, maadui wamegonga mwamba katika mpango wao wa kuusambaratisha uchumi wa Iran ya Kiislamu.

Rais Rouhani ameongeza kuwa: Maadui walikuwa wakidhani kwamba, kwa kushadidisha vikwazo, watawafanya wananchi wa Iran wapoteze matumaini na wataifanya serikali ishindwe kutekeleza mipango yake, lakini maadui hao wameshindwa na wamekata tamaa.

Rais Hassan Rouhani (kulia) akimkabidhi Spika wa Bunge Ali Larijani (wa mwisho kushoto) ripoti ya bajeti

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa: Kama walivyotaka wananchi na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, serikali ya Iran imepiga hatua za kuridhisha katika masuala makuu ya uchumi; na nchi inaelekea kwenye maendeleo na ustawi.

Aidha amesema: Ishara na makadirio yanaonyesha kuwa katika mwaka huu, ukuaji wa uchumi wa Iran bila kutegemea mafuta utakuwa wa hali chanya na akaongeza kuwa: Bajeti ya mwaka ujao, kwa sehemu kubwa haitakuwa tegemezi kwa mapato ya mafuta.../

Tags

Maoni