Dec 10, 2019 14:04 UTC
  • Spika Larijani: Iran inaendelea kustawi licha ya vikwazo

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani amesema kuwa, Iran inaendelea kustawi pamoja na kuwa imewekewa vikwazo.

Larijani ameyasema hayo alipozindua miradi sita ya usambazaji maji katika mkoa wa Kermanshah magharibi mwa Iran leo Jumanne.

Aidha amesema kuwa, Iran hivi sasa inakabiliwa na hali ngumu kutokana na vikwazo shadidi lakini pamoja na hayo miradi ya maendeleo inaendelea kuzindiliwa na pia miradi ya kiviwanda haijasimama. 

Larijani aidha amesema kuwa taifa la Iran lina matumaini tele kuwa litaweza kufanikiwa katika kusimama kidete mbele ya maadui.

Amesema taifa linaweza kusimama kidete mbele ya maadui pale linapokuwa na matumaini.

Wiki iliyopita, Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema, Marekani inapaswa ijijue kwamba si kiongozi wa dunia bali ni nchi kama zilivyo nchi zingine na akasisitiza kwamba, vikwazo vya Marekani ni kosa kubwa la kisiasa na kiuchumi na ni hatua iliyo dhidi ya kanuni na maazimio ya kimataifa.

Akizungumza wakati wa kupokea hati za utambulisho za Bi Lyndall Sachs, balozi mpya wa Australia hapa nchini, Rouhani alibaini kuwa nchi zenye misimamo huru na zinazojitegemea zinapasa kusimame imara kukabiliana na hatua zisizo za kisheria za Marekani.

Rais Rouhani alisema kuwa, Marekani haitaweza kufikia malengo yake kwa kuweka vikwazo na kuongeza kwamba: Taifa la Iran ni taifa kubwa na wala halitishiki kwa mashinikizo ya aina hiyo.

Maoni