Dec 13, 2019 00:44 UTC
  • Aghalabu ya waliouawa katika ghasia za Iran, hawakuwapo kwenye maandamano

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema asilimia 85 ya watu waliouawa katika ghasia za hivi karibuni hapa jijini Tehran hawakuwepo kwenye maandamano au mikusanyiko yoyote, bali walilengwa na watu fulani kwa niaba ya maadui.

Ali Shamkhani alisema hayo jana Alkhamisi alipokutana na familia za wahanga wa ghasia hizo katika miji ya magharibi ya mkoa wa Tehran na kuongeza kuwa, "Aghalabu ya waliouawa katika mkoa wa Tehran wakati wa fujo hizo hawakuwapo kwenye maandamano au mijumuiko ya aina yoyote. Bila shaka kuna njama zilipikwa na maadui wa taifa hili ili kuongeza idadi ya waliouawa."

Ametoa mwito kwa magavana wote hapa nchini kufanya uchunguzi wa mauaji hayo ya raia na maafisa usalama, mbali na kuhakikisha kuwa familia za wahanga wa ghasia hizo na wale waliopoteza mali zao kwenye fujo hizo wanapewa fidia.

Kwa mujibu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, akthari ya wafanya ghasia za hivi kariuni walitiwa mbaroni wakati wakijaribu kutoroka Iran.

 

Moja ya mabenki yaliyoshambuliwa na wafanyafujo katika maandamano ya Iran

Itakumbukwa kuwa, hatua ya kuifanyia marekebisho bei ya mafuta ya petroli nchini Iran hapo Novemba 15 mwaka huu, ilipelekea kuibuka maandamano ya amani ya wananchi mjini Tehran na baadhi ya miji mingine ya nchi.

Hata hivyo kundi fulani la wafanya ghasia na ambalo lilipewa mafunzo na maadui wa Iran, lilijipenya katika maandamano hayo na kuanza kuharibu mali za umma na za watu binafsi zikiwemo benki, idara, magari ya kubeba wagonjwa na magari ya usafiri.

 

Tags

Maoni