Dec 14, 2019 12:31 UTC
  • Mousavi: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni sawa na jinai dhidi ya binadamu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfano wa wazi wa jinai dhidi ya binadamu na ugaidi wa kiuchumi.

Sayyid  Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo Jumamosi wakati akizungumza na waandishi habari mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Mousavi amepinga madai ya Marekani kuwa Iran haijawekewa vikwazo vya dawa na chakula na kusema: "Mashirika ya Iran yanayonunua dawa au bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi hukumbwa na matatizo  ya kuhamisha pesa kwa njia ya benki."

Mousavi amebaini kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vimekiuka haki za binadamu na sheria zote za kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amesema Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatazamiwa kuitembelea Japan hivi karibuni na kusema: "Japan, ambayo kwa nia njema imewasilisha mapendekezo ya kupunguza taharuki, inataraji kuwa safari ya Rouhani nchini humo itazaaa matunda mema kwa nchi mbili."

Waziri Mkuu wa Japan Abe Shinzo (kushoto) na Rais Hassan Rouhani wa Iran walipokutana mjini Tehran, Juni 12 2019

Mousavi aidha amesisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa Iran na nchi zote zikiwemo nchi jirani na kuongeza kuwa: "Baadhi ya nchi jirani hazina uhusiano mzuri na Iran kutokana na matatizo yao ya ndani lakini baadhi ya nchi zina nafasi ya kipekee katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria matokeo ya uchaguzi wa Alhamisi nchini Uingereza na kusema: "Serikali mpya ya Uingereza, pamoja na Umoja wa Ulaya, na serikali za Ufaransa, Ujerumani, Russia na China, zinapaswa kuchukua hatua za kivitendo za kufungamana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA."

 

Maoni