Jan 16, 2020 02:30 UTC
  • Sisitizo la Iran la kutoa jibu kali kwa ukiukaji wa ahadi na kwa hatua hasi za nchi tatu za Ulaya kuhusu mapatano ya JCPOA

Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa radiamali sambamba na nchi tatu za Ulaya kuamua kutekeleza utaratibu wa kutatua hitilafu katika mapatano ya JCPOA na kueleza kuwa hatua hiyo si ya uwajibikaji na imechukuliwa katika hali ya udhaifu.

Mousavi amebainisha kuwa: Tutajibu vikali na kwa uzito kamili ukiukaji wa ahadi na hatua hasi za nchi tatu za Ulaya. 

Ujerumani, Uingereza na Ufaransa nchi tatu zinazounda "Troika ya Ulaya" Jumanne wiki hii zilitoa taarifa mjini Brussels Ubelgiji zikibainisha kuwa zimeamua kutekeleza utaratibu wa kutatua hitilafu ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Kutangazwa  na upande wa Ulaya uamuzi wa kuanzisha mchakato huo wa kutatua hitilafu ndani ya mapatano ya JCPOA na kutekeleza kipengee cha 36 cha mapatano ya JCPOA kunajiri katika hali ambayo kipengee hicho kilishazungumziwa tangu huko nyuma na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia jambo hilo akisema: Tangu mwaka mmoja na ushei  uliopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alituma barua kadhaa rasmi kwa Mratibu wa Kamisheni ya Pamoja ya Mapatano ya JCPOA na kuanzisha mchakato wa kuzipatia ufumbuzi hitilafu ndani ya mapatano hayo. Kwa hiyo hakuna jipya lililotokea, si katika upande wa  kimchakato wala upande wa utekelezaji wa kivitendo.  

Pande za Ulaya ndani ya mapatano ya JCPOA hazijachukua hatua yoyote ya maana na ya jadi licha ya majukumu ziliyokuwa nayo kwa mujibu wa mapatano hayo na baada ya Marekani kujitoa katika JCPOA na pande hizo kuongoza rasmi vikao mbalimbali vya Kamisheni ya Pamoja ya mapatano hayo.

Kipengee cha 36 cha mapatano ya JCPOA kinaeleza hivi: "Iwapo Iran itaamini kuwa upande mmoja au kundi zima la 5+1 halijatekeleza majukumu yake; inaweza kuwasilisha suala hilo kwa Kamisheni ya Pamoja kwa ajili ya kupatia ufumbuzi. Kwa utaratibu huo huo, iwapo nchi moja au kundi zima la wanachama wa 5+1 zitajiaminisha kwamba Iran nayo haijaheshimu ahadi zake ndani ya mapatano hayo kila serikali ndani ya kundi hilo la 5+1 pia inaweza kuchukua hatua sawa na hiyo.   

Pande za Ulaya zimedai katika taarifa yao ya karibuni kwamba kuanza mchakato wa kuzipatia utatuzi hitilafu ndani ya JCPOA kunatekelezwa kwa njia njema na kwa lengo ya kuyalinda mapatano hayo ya nyuklia na zinataraji kuwa itapatikana njia ya kuvuka mkwamo uliojitokeza kupitia kufanyika mazungumzo muhimu ya kidiplomasia. Pande hizo zimesisitiza kuwa hazijiungi na kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya Marekani dhidi ya Iran katika kutekeleza shughuli hiyo. 

Mikhail Ulyanov Mwakilishi wa Russia katika Taasisi za Kimataifa ametoa radiamali yake kuhusu uamuzi huo wa nchi tatu za Ulaya wanachama wa mapatano ya JCPOA na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Anataraji kuwa uamuzi huo wa Ulaya hautaifanya hali ya mambo ya sasa kuwa tete zaidi. Baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja kwenye mapatano hayo ya nyuklia; Iran imefanya juhudi za kuyalinda kwa sharti kwamba pande nyingine nazo zitekeleze ahadi na majukumu yao kwa mujibu wa mapatano hayo.

Mikhail Ulyanov, Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa 

Aidha ikiwa imepita karibu miaka miwili sasa, pande za Ulaya hazijatekeleza hatua yoyote ya kuzingatiwa mkabala na zinavyopaswa kuwajibika kwa mujibu wa mapatano hayo. Sababu hiyo imeipelekea Iran kuanza kupunguza uwajibikaji wake ndani ya JCPOA katika muda wa siku sitini kulingana na haki iliyonayo katika fremu ya makubaliano hayo ya nyuklia. Kwa mujibu wa haki yake hiyo, mnamo tarehe 5 mwezi huu, Iran ilitoa taarifa ikitangaza kuanza kutekeleza hatua yake ya tano ya kupunguza uwajibikaji wake ndani ya mapatano ya JCPOA ambapo kwa mujibu wake, Tehran haitakuwa tena na vizuizi katika uga wa utekelezaji ikiwemo kiwango cha urutubihsaji urani, asilimia ya urutubishaji, kiwango cha mada zilizorutubishwa na katika upande wa utafiti na ustawi; na kuanzia hapo shughuli za nyuklia za Iran zitaendelezwa kwa mujibu wa mahitaji yake ya kiufundi na ushirikiano kati yake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) pia utaendelea kama kawaida. 

Wakati huo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa kama ilivyokuwa huko nyuma iko tayari kikamilifu kuonyesha nia njema mkabala na nia njema yoyote itakayoonyeshwa kwake na kwa juhudi za kimantiki zitakazofanywa kwa ajili ya kuyalinda mapatano hayo ya kimataifa. Hata hivyo imesema itatoa jibu linalofaa na kali kwa hatua yoyote ya kutowajibika, yenye nia mbaya na isiyofaa kuhusiana na mapatano hayo ya nyuklia.  

Msimamo wa Iran katika uwanja huo uko wazi. Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: Nchi tatu za Ulaya zinaweza kunusuru mapatano ya JCPOA lakini si kwa kuipigia magoti Marekani na kuushinikiza upande uliowajibika (Iran) bali inapasa ziwe na uthubutu wa kutekeleza majukumu yao. 

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Nukta muhimu ni kuwa wanasiasa na wapangaji sera kuanzia Brussels hadi London na Berlin wote wanataka kulindwa mapatano ya JCPOA; hata hivyo mapatano hayo hayawezi kulindwa kwa maneno matupu. Badala ya kutosheka na utoaji taarifa tu, nchi za Ulaya zinapaswa kuthibitisha kuwa zina irada huru na ya kujitegemea ya kulinda utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande kadhaa.

 

Maoni