Jan 16, 2020 11:23 UTC
  • Zarif: Ulaya wameamua

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika ujumbe mkali katika mtandao wa kijamii wa Twitter kulaani udhaifu wa nchi za Ulaya mbele ya Marekani na kuandika: Nchi tatu za Ulaya zilizobakia kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA zimeamua kuyatupa makubaliano hayo kwa kuhofia ushuru mpya ambao Trump ametishia kuziwekea ushuru mpya nchi za Ulaya.

Idara Kuu ya upashaji habari ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran leo Alkhamisi imenukuu ujumbe huo wa Twitter wa Dk Mohammad Javad Zarif akiwaambia viongozi wa Ulaya kwamba: "Nyinyi hamna ubora wowote wa kimaadili na kisheria."

Ujumbe huo wa Twitter wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha umesema, udhaifu wa nchi za Ulaya wa kung'ang'ania kuiridhisha Marekani kwa hali yoyote ile, hauna manufaa kwa nchi hizo bali utazidi tu kuongeza tamaa ya rais wa Marekani, Donald Trump. 

Dk Zarif amewahutubu viongozi wa nchi hizo tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani akiziambia: Je, bado mnakumbuka ubabe wa kipindi cha shule za sekondani? Hivyo kama mnataka kuuza heshima yenu basi endeleeni na njia hiyo hiyo lakini msidai kuwa mna ubora wa kimaadili na kisheria, hamna ubora huo. 

Wakuu wa troika ya Ulaya wanaoogopa ushuru mpya wa Trump

 

Nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa siku ya Jumanne ziliamua kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Kwa mujibu wa mchakato huo, iwapo nchi yoyote kati ya zilizofikia makubaliano hayo itadai kuwa upande fulani umekanyaga mapatano hayo, suala hilo hutakiwa kupitia hatua takriban ndefu za kuchunguza madai hayo na mwishowe kuchukuliwa uamuzi unaofaa.

Nchi za Ulaya zinadai kuwa, hatua ya Iran ya kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA ni kukiuka mapatano hayo, wakati Iran inasema kuwa, nchi za Ulaya zimeshindwa kutekeleza ahadi zao baada ya Marekani kujitoa na wala hazikabiliani na vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Iran na Marekani. Tehran inasema,  kupunguza ahadi zake katika JCPOA kumefanyika kwa mujibu wa sheria na wala si kukiuka vipengee vya mapatano hayo.

Tags

Maoni