Jan 16, 2020 15:22 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Iran: Marekani imesalimu amri moja kwa moja kwa uwezo mkubwa wa Iran katika uga wa makombora

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia jibu kali la makombora ya nchi hii dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani, kufuatia jinai ya Washington ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC na kusema kuwa suala hilo limebainisha uhalisia wa uwezo mkubwa wa makombora wa taifa hili uliomfanya adui asalim amri mbele ya Iran.

Brigedia Jenerali Amir Hatami ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Maafisa wa Kijeshi cha Imam Ali (as) katika kuwaenzi wanafunzi 1,184 wa chuo hicho hususan Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, na kuongeza kuwa shambulizi la makombora la Iran kwenye kambi ya jeshi la Marekani ya Ain Assad nchini Iraq, ni ishara ya wazi ya uwezo, irada na azma ya moja kwa moja ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya adui. Aidha Brigedia Jenerali Amir Hatami sambamba na kubainisha hatua ya Marekani ya kutekeleza ugaidi wa kiserikali ambao ulikuwa haujawahi kushuhudiwa duniani hasa kutokana na kumuua shahidi kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la nchi fulani akiwa mgeni rasmi wa serikali ya nchi nyingine, ni kitendo kichafu sana na kubainisha kuwa, suala kuu la uadui wa Washington dhidi ya taifa la Iran, unatokana na nchi hii ya Kiislamu kujitegemea yenyewe.

Sehemu ndogo ya makombora hatari ya Iran ya Kiislamu yaliyoipigisha magoti Marekani

Waziri wa Ulinzi wa Iran ameongeza kwamba mfumo wa kibeberu sambamba na kufanya njama kubwa zenye lengo la kuibua mpasuko katika uga wa kiutamaduni kati ya nchi za eneo la Asia Magharibi, kuunda makundi yenye mafungamano na uga wa kisiasa na adui, kuzitwisha nchi kadhaa mzigo wa matatizo ya kiuchumi, njama ya kuzigawa nchi za eneo kwa msingi wa kijografia na kupandikiza utawala wa saratani yaani utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndani ya eneo hili, yote hayo yana lengo la kuleta mabadiliko kuelekea upande wa kutapakaza fitina kubwa. Usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 mwezi huu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye alikuwa ameelekea nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, akiwa pamoja na Naibu Mkuu wa harakati ya Al-Hashdu-Sha'abi Abu Mahdi Al-Muhandis na wanamuqawama wengine wanane waliuliwa shahidi baada ya msafara wa magari yaliyowabeba kulengwa na makombora ya majeshi ya kigaidi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Katika kujibu jinai hiyo ya kigaidi ya Marekani, siku ya Jumatano iliyofuatia Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilishambulia kwa makumi ya makombora kambi za jeshi la Marekani katika mkoa wa Al-Anbar na Erbil nchini Iraq.

Maoni