Jan 17, 2020 03:30 UTC
  • Meja Jenerali Baqeri: Marekani itapata jibu kali zaidi la Iran ikiendeleza mienendo yake hasi

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema iwapo Marekani itaendeleza chokochoko na mienendo yake hasi dhidi ya taifa hili, basi iwe tayari kupokea jibu kali zaidi la Iran ya Kiislamu.

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar ambapo alieleza bayana kuwa: "Hatua ya Washington ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC ilikuwa ya kioga, isiyo na utu na inayokinzana na sheria na kanuni zote za kimataifa."

Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haioni umuhimu wowote wa kushadisisha taharuki katika eneo la Asia Magharibi, lakini haitasita kutoa jibu kali kwa hatua yoyote ya kichokozi ya adui na kwamba, "inatarajiwa kuwa, mizizi yote ya fitina na migogoro katika eneo itang'olewa kwa kuondoka Marekani katika eneo hili."

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar sanjari na kukosoa kitendo cha Marekani cha kumuua shahidi Jenerali Soleimani pamoja na wafuasi wake, amebainisha kuwa: "lazima tushirikiane bega kwa bega kuimarisha uthabiti katika eneo, na tusiruhusu makundi ya kigaidi yatumie vibaya taharuki inayoshtadi kila uchao katika eneo."

Jenerali Baqeri (wa pili kutoka kulia) na Hulusi Akar alipoitembelea Iran

Hiyo jana pia, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizungumzia jibu kali la makombora ya nchi hii dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani, kufuatia jinai ya Washington ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC na kusema kuwa suala hilo limebainisha uhalisia wa uwezo mkubwa wa makombora wa taifa hili uliomfanya adui asalimu amri mbele ya Iran.

Siku chache baada ya majeshi ya kigaidi ya Marekani kumuua shahidi Jenerali Soleimani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad tarehe 3 mwezi huu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilishambulia kwa makumi ya makombora kambi za jeshi la Marekani katika mkoa wa Al-Anbar na Erbil nchini Iraq.

Tags

Maoni