Jan 17, 2020 12:32 UTC
  • Iran na India; juhudi kwa ajili ya kutumia sarafu ya taifa na kupanua ushirikiano wa kiuchumi

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo mjini New Delhi na Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India na kujadili suala la kupanua ushrikiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili na kuchukua hatua za kuondoa baadhi ya matatizo yaliyopo katika njia hiyo.

Dakta Muhammad Javad Zarif alisema jana Alkhamisi baada ya kukamilisha mazungumzo yake na viongozi wa ngazi za juu wa India kwamba, kumefikiwa makubaliano baina ya pande mbili kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kiuchumi kati ya Tehran na New Delhi. Dakta Zarif amesema: Mbali na kuanzishwa Benki ya Kiirani nchini India, pande mbili zimekubaliana pia kufunguliwa tawi moja la Benki ya India katika Bandari ya Chabahar iliyoko kusini mashariki mwa Iran.

Iran na India ambazo zina ushirikiano mzuri wa kiuchumi, zimekuwa zikifanya juhudi za kutumia mbinu za kitaifa ili kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani kwa minajili ya kutatua matatizo yaliyopo katika ushirikiano wa kiuchumi.

Kutumia sarafu ya taifa ni mbinu mbadala katika mabadilishano ya kifedha baina ya Iran na India ambayo inapewa kipaumbele na nchi mbili hizi na kuhusiana na kadhia hiyo, kuanzishwa shughuli za kibenki za Iran nchini India na Benki ya India nchini Iran bila shaka ni jambo la dharura. Kutatua tatizo la mabadilisho ya kifedha kati ya Iran na India ni jambo muhimu ili kwa kutumia mipango na mbinu zilizoafikiwa, kupunguzwe kivuli cha mamlaka na satua ya sarafu ya dola katika mabadilishano ya kifedha.

Bendera za Iran na India

Kutumia sarafu ya taifa katika mabadilishano ya kifedha na kiuchumi baina ya Iran na mataifa mengine ni jambo linalozingatiwa mno na viongozi wa Tehran. Kabla ya hapo ilitangazwa kuwa, baadhi ya mabadilishano ya kifedha na kiuchumi ya Iran na nchi za Uturuki, Russia na Iraq yamekuwa yakifanyika kwa kutumia sarafu ya taifa, ambapo hatua hiyo imepelekea kutokea mabadiliko muhimu katika ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili na pande kadhaa bila ya sarafu ya dola kuwa na nafasi.

Hii leo watu wote wanaamini kwamba, matumizi ya sarafu ya dola katika mabadilishano ya kibiashara ulimwenguni yametawaliwa na matashi ya kisiasa. Kupunguza mamlaka na satua ya sarafu ya dola ya Marekani katika mabadilishano ya kifedha na kiuchumi duniani ni jambo linaloungwa mkono na madola huru ya dunia na yasiyokubali kuburuzwa ambayo yanafuatilia suala la ustawi na ushirikiano wa kiuchumi bila kuingiza matashi ya kisiasa.

Katika fremu hii, Iran na India zikiwa nchi mbili mbili na athirifu katika mahesabu ya eneo na kimataifa, zinafanya hima ya kuweko mbinu mbadala ya dola ili kuondoa satua na mamlaka ya sarafu ya dola katika mabadilishano yao ya kibenki na kiuchumi.

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran (kushoto) akiwa na Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India

Makubaliano ya kuanzisha tawi la Benki ya Iran ya Pasargad nchini India na kufungua tawi la Benki ya India katika bandari muhimu ya Chabahar ya Iran ni ishara ya kuweko irada na azma thabiti ya nchi mbili kwa ajili ya kudumisha ushirikiano wa kiuchumi na kuondoa vizingiti vilivyoko katika mabadilishano ya kifedha baina ya pande mbili.

Katika fremu hii, uwepo na uwekezaji wa India katika Bandari ya Chabahar iliyoko kusini mashariki mwa Iran ni jambo muhimu na la kiistratijia kwa Wahindi ili kwa njia hiyo waweze kulifikia soko jipya.

Kwa kuzingatia kwamba, Bandari ya Chabahar ina fursa ya dhahabu ya kiuchumi kwa India, New Delhi inafanya juhudi za kila namna licha ya kuweko vikwazo vya Marekani ili ipanue ushirikiano wake wa kiuchumi na Iran. Makubaliano ya kuanzisha tawi la Benki ya India huko Chabahar kusini mashariki mwa nchi  yaliyofikiwa katika safari ya Dakta Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika mji mkuu wa India, New Delhi yanaweza kutathminiwa katika uwanja huu.

Tags

Maoni